Tetemeko: Phoebe Oketch athibitisha yeye na wenzake 2 wa Harambee Starlets wako salama nchini Uturuki

Tetemeko: Phoebe Oketch athibitisha yeye na wenzake 2 wa Harambee Starlets wako salama nchini Uturuki

NA AREGE RUTH 

WACHEZAJI watatu wa Harambee Starlets mshambuliaji Mwanahalima Adams, mabeki Vivian Nasaka na Phoebe Oketch ambao wanachezea timu ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Hakkarigücü Spor nchini Uturuki, wako salama baada ya tetemeko kubwa la ardhi kusababisha uharibifu mkubwa nchini humo na katika taifa jirani Syria.

Timu hiyo yenye maskani yake Hakkari ambayo iko kusini-mashariki mwa Uturuki, haikuathiriwa na janga hilo.

Tetemeko hilo ambalo limefanyika mapema wiki hii, kufikia sasa, zaidi ya watu  11,000 kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria wameaga dunia.

Kanda za kuhuzunisha zimeibuka za uokoaji.

Miongoni mwa waliookolewa ni Mchezaji wa kimataifa wa Ghana Christian Atsu anayechezea klabu ya Uturuki ya Hayatspor.

Mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea ya Uingereza, aliripotiwa kupotea ghafla siku ya Jumatatu kabla ya kuokolewa. Taarifa zinasema, sasa amelazwa hospitalini akiwa na jeraha la mguu na matatizo ya kupumua.

Akizungumza na Taifa Spoti Phoebe ambaye yuko nchini Uturiki ameelezea kuwa, hata ingawa hawajaathiriwa na janga hilo, kwa sasa wamechukua mapumziko mafupi hadi hali ya kawaida itakaporejea.

“Siku ya Jumanne usiku tulisikia mtetemeko kwenye jumba letu. Tulilazimika kukesha nje hadi kuchelewa, tulihofia huenda tungeangukiwa na jengo hilo. Pia, hakuna timu yoyote ya soka ya wanawake iliyoathiriwa,” alisema Phoebe.

“Sisi Wakenya tunaishi sehemu moja. Hatuendi mazoezini, tumechukua mapumziko mafupi kutokana pia na theluji ambayo imetanda kila mahali.  Tumejifungia tu katika vyumba vyetu, lakini tuko salama,” aliongezea Phoebe.

Rais wa 12 wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, akizungumza na vyombo vya habari nchini humo alisema, hali sasa inaendelea kuwa bora zaidi ikilinganishwa na siku tatu za nyuma.

“Hapo awali shughuli zilisitishwa katika viwanja vya ndege na barabara za kupitia magari lakini hali inaendelea kurejea kawaida. Tumekusanya rasilimali zetu zote na kila jimbo linafanya kazi yake,” Erdogan anasema.

Miji iliyoathiriwa ni Hatay, Diyarbakir, Kahramanmaras, Gaziantep, Adana, Adiyaman, Sanliurfa, Malatya, na Mardin.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Sakaja aahidi kuwaajiri maafisa wa kitengo cha...

Pwani: Kuna haja wazazi, serikali kulinda watoto dhidi ya...

T L