HabariMichezo

The Lions of Teranga watafuna na kumeza Lewandowski na wenzake

June 19th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

HATIMAYE bara zima la Afrika limenguruma, vigelegele vimetanda kote barani miongoni mwa mashabiki kindakindaki wa mchezo wa soka baada ya Senegali ‘The Lions of Teranga’ kunguruma na kuwala Poland mabao 2-1.

Timu hiyo iliwarejeshea matumaini mashabiki  Wafrika baada ya mlinzi wa Poland Thiago Cionek kujifunga huku kipindi cha kwanza kikiisha Senegal wakiongoza 1-0.

Katika kipindi cha pili mshambulizi wa Senegali M’baye Niang’ alitia msumari moto kwenye kidonda cha Poland kwa kuongeza bao la pili wakati kipa wa Poland aliposhindwa kumakinika kuondoa mpira katika eneo hatari.

Bao la kufuta machozi la Poland lilifungwa dakika ya 86 na mchezaji wa Poland Grzgorz Krychowiak.

Matokeo hayo yanajiri baada ya wawakilishi wengine wa bara Afrika kusalia gumegume na wakawa mbumbumbu mzungu wa reli mbele ya wapinzani.

Ilikuwa aibu iliyoje nchi zilizotegemewa kama Nigeria, Misri, Tunisia, Morocco kutosajili ushindi wala sare yoyote katika mchuano uliokuwa ukifuatiliwa kwa makini na mamilioni mwa mashabiki kutoka pembe yote ya ulimwenguni.

Nigeria maarufu kiama ‘Super Eagles’ waliowekewa nafasi kubwa kati ya timu hizo kutamba walishindwa kuifunga Croatia katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia.

Licha kujivunia huduma za mastaa kama Obi Mikel, Victor Moses na Alex Iwobi, mibabe hao wa soka ya Afrika walikubali kichapo cha 2-0 mikoni mwa Croatia.

Timu hiyo kutoka Magharibi mwa Afrika bado ina mlima mrefu wa kuukwea katika kundi lao na itapiga hatua tu iwapo itaishinda Argentina na Jamuhuri ya Ice land ambao ndiyo wapinzani wao waliosalia.

Kwa upande wao, Misri walilimwa na Urusi 3-1 licha ya kuwa na mshambuliajia matata Mohamed Salah kwa kikosi, hali iliyozima matumaini ya taifa hilo la uarabuni kutinga 16 bora.