Michezo

‘The Reds’ moto kama pasi

January 31st, 2020 2 min read

 GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

LIVERPOOL iliendeleza kampeni yake safi msimu huu baada ya kuchabanga wenyeji West Ham 2-0 uwanjani London mnamo Jumatano ikijizolea ushindi wake wa 19 kwenye Ligi Kuu, ambayo ni rekodi mpya ya klabu hiyo.

Timu hiyo almaarufu ‘The Reds’, ilichukua uongozi kupitia penalti ya Mohamed Salah dakika ya 35 baada ya Issa Diop kuangusha Divock Origi ndani ya kisanduku.

Liverpool ilimiliki mpira kutoka kipenga cha kwanza na kudhibiti mchezo kwa kipindi kikubwa, ingawa ilipata bao la pili baada ya kuzima shambulio la West Ham.

Mara hii, Salah aligeuka kuwa muundaji wa nafasi hiyo akimegea Alex Oxlade-Chamberlain pasi murwa nyuma ya walinzi wa West Ham kabla ya Muingereza huyo kuchomoka kama risasi na kufikia mpira huo na kisha kusukumia Lukasz Fabianski kombora kali ambalo kipa huyo hakuweza kulipangua.

Ushindi huo uliwezesha Liverpool kufungua mwanya wa alama 19 juu ya jedwali dhidi ya wapinzani wake wa karibu Manchester City, ambao wanashikilia nafasi ya pili na pia ni mabingwa watetezi.

Liverpool, ambayo imezoa alama 70 (imesakata mechi 24 sawa na wengine), sasa haijapoteza ligini katika mechi 41 mfululizo tangu msimu uliopita.

Ushindi dhidi ya West Ham unamaanisha kuwa Liverpool sasa imepepeta kila mpinzani kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 127 ya Liverpool imepata mafanikio kama hayo kwenye Ligi Kuu na ilihitaji mechi 24 pekee kuyapata.

Hata hivyo, Liverpool ilipata ufanisi sawa na huo msimu 1894-1896 ilipokuwa katika Ligi ya Daraja ya Pili, miaka 125 iliyopita.

Kuonyesha umuhimu wa mafanikio hayo ya Liverpool ni kuwa hata kikosi cha Arsenal kinachofahamika kama Invincibles hakikufikia kiwango hicho kwa sababu hakikupiga Portsmouth na Manchester United.

Vilevile, Chelsea, chini ya kocha Jose Mourinho msimu 2004-2005, ilishindwa kupiga Manchester City na Arsenal, ingawa timu ya City ya kocha Pep Guardiola ya msimu 2017-2018, ambayo inashikilia rekodi ya kushinda mara nyingi ligini katika msimu mmoja, ilifaulu.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp itaalika timu ya Southampton, ambayo imeamka, uwanjani Anfield hapo kesho. Vijana wa Klopp watalenga kuendelea kuvizia rekodi ya Arsenal kutoshindwa msimu 2003-2004, ambayo ni mechi 49.

Mabingwa mara 18 Liverpool, ambao wanatafuta taji lao la kwanza la Ligi Kuu katika kiopindi cha miaka 30, wamebakisha mechi nane wafikie rekodi ya kutoshindwa ya Arsenal iliyowekwa kutoka Mei 7, 2003 hadi Oktoba 24, 2004.