Habari MsetoKimataifaSiasa

Theresa May atua Kenya

August 30th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

WAZIRI Mkuu wa Uingereza Theresa May tayari ametua Kenya kwa ziara ya kitaifa, miaka 30 baada ya Waziri Mkuu wa zamani nchi hiyo Margaret Thatcher kuzuru humu nchini.

Bi May alitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa kumi na mbili alfajiri akitumia ndege yake rasmi, baada ya kuzuru Nigeria Jumatano.

Alifika pamoja na kikundi cha wafanyabiashara na wawekezaji walio tayari kufanya biashara na Kenya na Afrika kwa jumla.

Waziri Mkuu huyo na Rais Uhuru Kenyatta wanatarajiwa kufanya kikao cha pamoja na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi saa tano asubuhi.

Bi May anatarajiwa kukutana na Rais Kenyatta kabla ya kuwatembelea wanajeshi wa Uingereza walio humu nchini na shule moja ya kibiashara.

Kisha ziara yake itakamilishwa na chajio kitakachoandaliwa na serikali.

“Ninajivunia kuongoza ziara hii yenye matumaini Afrika na kuwa Waziri mkuu wa kwanza wa UK katika kipindi cha miaka 30 kuzuru Kenya,” Bi May akasema kabla ya ziara.

Bi Thatcher alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo kutembelea Kenya mnamo 1988.