Michezo

Theta United FC yajiandaa kwa ligi ya Thika msimu ujao wa 2020

October 1st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

INGAWA hawajashiriki katika michuano yoyote ya ligi, chipukizi wa Theta United FC wanaamini siku yao bado yaja na wako tayari kwa lolote.

Kocha John Kamau anadai kuwa klabu hiyo ina maazimio makuu licha ya changamoto tele; hasa pandashuka kwa miaka mitatu na nusu tangu ibuniwe.

“Bado ndoto yetu iko imara huku tukipania kukwea milima na mabonde,” anasema kocha huyo mwenye matumaini makubwa.

Anasema matarajio yake kwa sasa ni kuinua kikosi hicho huku akilenga kushiriki ligi ya kaunti ndogo ya Thika ifikapo msimu ujao wa 2020.

“Nimejaribu kuongea na baadhi ya kampuni pamoja na mashirika binafsi na ninaamini kwamba huenda wakajibu maombi yetu na hivyo timu kupata udhamini,” anasema kocha Kamau.

Aidha, anasema hata mashabiki sugu na wazazi kadha wa vijana hao wanaendelea kuweka mikono yao pamoja ili kuhakikisha timu hiyo inaafikia malengo yake makuu.

“Tunalenga kupigana kufa kupona kwenye kampeni zetu kujiongezea maarifa kabla ya kujitosa katika kibarua kilicho mbele yetu kupanda ngazi ya Ligi,” anasema mkufunzi.

Matokeo

Katika majuma machache yaliyopita timu hiyo imecheza na timu kadha.

Theta United iliibomoa Juja Farm FC kwa mabao 2-0.

Vijana hao waliizaba Kiaora Stars mabao 2-1.

Chipukizi hao walitoka sare na Benniver kwa kulimana 1-1.

Hata hivyo, ilipoteza mechi yake dhidi ya Gachororo FC kwa kulala magoli 2-1.

Hapo awali timu hiyo ilishiriki taji la Kalimoni Youth Cup, ambapo ilijikwaa kwenye nusu fainali mikononi mwa Benniver iliyowaadhibu 2-1.

Katika robo fainali ilikuwa imeipepeta Juja Farm mabao 2-0.

“Licha ya kupambana na kuendesha timu hiyo wakazi wa Juja na vitongoji vyake wanajivunia kuwa na timu yao ya mitaani,” anasema Kocha huyo.

Anatoa wito kwa Wizara ya Michezo ya Kaunti ya Kiambu kujitokeza angalau kuwapiga jeki ili wanawiri.

“Tayari tumepata mialiko katika Kaunti ya Murang’a na Kiambu ili tucheze mechi za kirafiki,” anasema Kamau.

Anaeleza kuwa changamoto za kukosa fedha na vifaa vya soka ndizo kikwazo kikubwa kilichoko mbele yao.

Kulingana na ratiba yake, kwa sasa anasema mazoezi yao hufanyika katika Uwanja wa Murera, Juja; kati ya Jumanne na Ijumaa huku wikendi wakishiriki mechi za kirafiki.