Michezo

Thika Allstars, Spitfire, PCEA Kikuyu zasubiri kukabana

April 26th, 2020 2 min read

NA JOHN KIMWERE

KAMPENI za kufukuzia taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili ni kati ya vipute vilivyoshuhudia kivumbi kikali kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

Mechi za kuwania ubingwa huo zimegawanywa katika makundi matatu ambapo timu zitakaomalia kileleni zitakutanishwa katika fainali kusaka bingwa.

Kipute hicho kinashirikisha vikosi 42 zikiwa timu 14 kwa kila kundi.

Michezo ya Kundi B inaonekana zitaendelea kuwasha moto mkali ligi hiyo itakaporejea baada ya janga la virusi vya korona kufikia kikomo ambapo huenda mechi za tamati ndizo zitakaoamua mshindi.

Baadhi ya wachezaji wa Mwiki United

GEORGE MAKAMBI

Kabla ya kampeni hizo kukunjua jamvi, kocha wa timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), George Makambi alitaja kuwa kundi hilo litakuwa la kifo.

”Mlipuko wa virusi hatari vya korona ulichangia shughuli za ligi zote kote nchini kupigwa stopu ili kuthibiti maambukizi zaidi,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa bado wanatarajia kibarua kigumu ligi hiyo itakapoanza tena baada ya janga hilo.

THIKA ALLSTARS

”Misimu yote huanza ligi tukilenga kufanya kweli na kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza lakini mpango wetu huenda mrama tukikaribia kukamilisha mechi za mkumbo wa pili,” alisema kocha huyo na kuongeza kuwa uhaba wa ufadhili umeibuka donda sugu kwa kikosi hicho.

Baadhi ya wachezaji wa Kibra United

KNH inashikilia nafasi ya saba kwa alama 24 sawa na Water Works tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kuingia dimbani mara 15 kila moja.

Kikosi cha Thika Allstars kinaongoza kwa kuzoa alama 27, sawa na Spitfire FC na PCEA Kikuyu FC tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kila moja kuingia dimbani mara 15.

”Tulianza kampeni zetu vizuri kisha tulionyesha kivumbi kikali kwenye mechi za karibuni hali inayoashiria kuwa timu zote zimejipanga kupambana mwanzo mwisho,” alisema.

Kocha huyo anahimiza marefarii wawajibike na kutelekeleza jukumu lao ipasavyo bila kupendelea wanaposimamia mechi za kinyang’anyiro hicho ili kukuza soka kupaisha kiwango cha mchezo huo.

Timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH)

WAHISANI

”Tumekaa vibaya kwenye kampeni za muhula huu maana kikosi changu kinazikosa huduma za washambuliaji wazuri,” alisema meneja wa Mwiki United, Martin Momanyi na kuongeza kuwa katika mpango mzima ukosefu wa ufadhili ndio tatizo kuu.

Meneja huyo anatoa mwito kwa wahisani wajitokeza na kuwashika mkono kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wanasoka wanaoibukia.

Mwiki United imejikuta katika mduara hatari wa kushushwa ngazi maana imeshikilia nafasi ya 13 kwa alama tisa baada ya kushuka dimbani mara 14.

Orodha ya timu zinazoshiriki kipute hicho inajumuisha: Thika Allstars, Bomas of Kenya, Limuru Olympic, KNH, Muchatha United, Terror Squad, MRM FC, Kirigiti Community FC, PCEA Kikuyu, Mwiki United, Zetech Nyahururu, Waterworks, Kahawa United na Spitfire.