Habari Mseto

Thika Cloth Mills yapata zabuni ya kushona nguo za idara za serikali

July 3rd, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Thika Cloth Mills Ltd imepata zabuni ya kushona nguo za idara za serikali.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi Tejal Dodhia, Jumatano alimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwapa nafasi ya kujiendeleza kwa kazi hiyo.

“Tunaona juhudi za Rais za kuangazia ajenda zake nne miongoni mwao ikiwa ni kufufua viwanda. Sasa tunayo matumaini ya kuinuka kiuchumi,” alisema Bi Dodhia.

Alifafanua kwamba kiwanda hicho kilikuwa na wafanyakazi wapatao 2,000 hapo awali miaka za ’90 lakini hivi majuzi alirejesha wafanyakazi 700 nyumbani huku kampuni ikiwalipa nusu ya mishahara yao katika kile alikitaja ni “wakati mgumu wa janga la Covid-19.”

Hivi majuzi mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliwasilisha mswada bungeni ya kuitaka serikali itoze ushuru wa juu bidhaa kutoka nje ili kuokoa bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

Kulingana na mbunge huyo, wafanyabiashara wa sekta ya juakali wanastahili kuinuliwa kiuchumi kwa kupewa nafasi wauze bidhaa zao kwa bei nafuu ili wajiinue kifedha.

Kulingana na Bi Dodhia wa TCM, zabuni waliyopewa ni ya kushona nguo pamoja na barakoa za maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS).

“Hatua hiyo ya serikali italeta mwangaza katika biashara yetu ambayo imedorora kwa muda mrefu,” alisema Bi Dodhia.

Waandishi wa habari walipozuru kiwanda hicho mnamo Jumatano, walipata wafanyakazi wakiendelea kushona nguo zinazoashiria mwito wa ‘Nunua Kenya Jenga Kenya’.

Mkurugenzi huyo alipongeza Rais Kenyatta, kwa kuweka ahadi yake ya kuona ya kwamba viwanda hasa vya nguo, vinafufuliwa mara moja ili kushona barakoa na PPEs muhimu katika kusaidia kupunguza kuenea kwa Covid-19.

Alisema kampuni hiyo inashona baadhi ya nguo, zikiwa ni za oda spesheli kutoka kwa kiwanda cha KICOTEC cha Kaunti ya Kitui. Baadhi ya kazi ambazo wanasaidiana na kiwanda hicho ni pamoja na kushona barakoa za kupelekwa shuleni, na sare za machifu kote nchini.

Alisema licha ya hali ngumu, viwanda kadhaa vya nguo vitaweza kujikwamua.

“Janga la Covid-19 limeathiri wakulima wa pamba kutoka Ndalani, Machakos, Kituo, Homa Bay, Kisumu na hata Siaya. Lakini hata hivyo tutaendelea kuwapa usaidizi ili wazidi kujiendeleza kutokana na kilimo cha zao hilo,” alisema Bi Dodhia.