Michezo

Thika Queens na Vihiga Queens wamumunya wapinzani

April 16th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

THIKA Queens iliichabanga Soccer Queens kwa mabao 5-1 wakati Vihiga Queens ikisajili magoli 4-0 mbele ya Wadadia LG na kuendeleza mtindo wa kugawa dozi  kwenye mechi za Ligi Kuu ya Soka la Wanawake ya Kenya (KWPL) msimu huu.

Thika Queens iliteremka mjegoni kwa kazi moja kutesa na kuvuna ushindi  wa alama zote ili kulipiza kisasi cha kuzabwa mabao 4-0 na Oserian Ladies wiki iliyopita.

Thika ilitwaa ufanisi huo kupitia Mwanahalima Adams, Rachael Mwema, Catherine Wangechi, Nuru Hamadi na Fauzia Omar baada ya kila mmoja kupiga moja safi.

”Dah! Tumekaa vibaya msimu huu baada ya kuyeyusha pointi sita lakini bado tumepania kurekebisha makosa yetu ili kujituma kwa udi na uvumba kwenye juhudi za kufukuzia wapinzani wetu,” ofisa wa Thika Queens, Fredrick Chege alisema.

Nayo Mathare United Women ilipigwa na Oserian Ladies kwa mabao 5-0 huku Kisumu Allstars ikisonga mbele na kutua nne bora iliporarua Nyuki Starlets kwa mabao 4-2.

Wachana nyavu wa Spedag walidondosha mechi ya nane ilipocharazwa kwa mabao 4-0 na Kibera Girls Soccer Academy (KGSA), nayo GASPO Women na Trans Nzoia Falcons kila moja ilivuna bao 1-0 mbele ya Eldoret Falcons na Makolanders mtawalia.

Kwenye jedwali, mabingwa watetezi Vihiga Queens ingali kileleni kwa kufikisha alama 27, tano mbele ya Trans Nzoia Falcons na GASPO Women tofauti ikiwa idadi ya magoli.

MATOKEO YA MECHI ZOTE WIKENDI

Thika Queens                          5-1    Soccer Queens

Kisumu Allstars                       4-2      Nyuki Starlets

Kibera Girls Soccer Academy 4-0       Spedag

Mathare United Women          0-5      Oserian Ladies

Eldoret Falcons                       0-1      GASPO Women

Trans Nzoia Falcons               1-0     Makolanders

Wadadia LG                            0-4     Vihiga Queens