Michezo

Thika Queens wajiandaa kwa msimu mpya

August 14th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

HAKIKA msimu huu mambo siyo rahisi kwenye mechi za kufukuzia ubingwa wa Soka la Ligi ya Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL). Timu zinazoshiriki kampeni za kipute hicho zinazidi kutifua kivumbi kikali tofauti na ilivyokuwa msimu uliyopita.

Kusema kweli mambo ni vuta ni kuvute baina ya mahasimu wakuu katika mchezo huo hapa nchini. Malkia wa zamani, Thika Queens ni miongoni mwa vikosi vinavyoendelea kutesa kwenye mbio za migarazano ya muhula huu licha ya kufungua kampeni zake vibaya.

Kando na Thika Queens vita vya kuwania taji la msimu huu pia vinashirikisha mabingwa watetezi, Vihiga Queens, Gaspo Women FC, Kisumu All Starlets, Trans Nzoia Falcons inayoshiriki mechi hizo kwa mara ya pili bila kuweka katika kaburi la sahau kikosi cha Oserian Ladies. Oserian Ladies ya kocha, Hudson Odari pia Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) dah! ni ngumu kubashiri.

Thika Queens ya kocha, Benta Achieng raundi hii inajumuisha wachana nyavu wa umri mdogo hali inayoashiria bayana huenda ikaibuka moto wa kuotea mbali ndani ya miaka mitatu ijayo tofauti na ilivyo kwa sasa.

Ofisa wake mkuu, Fredrick Chege anasema ”Tumepania kuunda kikosi thabiti ambapo msimu huu unaweza kuchorea lakini muhula ujao tutakuwa levo nyingine.” Chege anadai waliachia wachezaji waliokomaa ili kuunda timu itakayosalia imara ndani ya misimu kadhaa ijayo baada ya kutwaa huduma za chipukizi ambao asimilia 80 yao wamo chini ya umri wa miaka 20.

Msimu uliyopita Thika Queens ilinasa huduma za mchezaji wa timu ya Harambee Starlets, Mwanahalima ‘Dogo’ Adams.

Kadhalika anasema kwa sasa hawaoni dalili za kubeba taji hilo baada ya kuteleza kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

”Katika mpango mzima Thika tumepania kukabili wapinzani wetu kwa udi na uvumba kufukuzia nafasi ya kumaliza kati ya tatu bora kwenye msimamo wa kipute cha msimu huu. Lakini kwa bahati mbaya mahasimu wetu wakiteleza tu pengine watakuta mwana siyo wao tena kwa kuzingatia tumekaa pazuri kufanya kweli,” alisema na kutoa onyo kwa wapinzani wao waanze kujipanga kwa shughuli za kufa mtu msimu ujao.

Warembo wa Thika walionyesha dalili za kuzinduka waliposhusha soka safi katika ardhi ya nyumbani na kuangusha wageni wao Vihiga Queens kwa mabao 2-1.

Kisha kwenye mechi za mkumbo wa pili, timu hiyo iliwasha moto mkali ugenini ilipolazimisha kutoka nguvu sawa magoli 3-3 dhidi ya mahasimu hao kwenye patashika waliokuwa wenyeji iliyopigiwa Uwanjani Mumias Sports Complex.

Kwenye jedwali ya kipute hicho, Thika Queens inafunga nne bora kwa kuzoa alama 46 baada ya kucheza mechi 20. Vihiga Queens inaongoza kwa alama 55, moja mbele ya Gaspo Women FC huku Trans Nzoia Falcons ikifunga tatu bora kwa kufikisha alama 49.

”Baada ya kibarua cha Vihiga Queens tunajiandaa kushiriki mechi tatu za nguo kuchanika tutakapokaribisha Gaspo Women na Trans Nzoia Falcons bila kusahau wenyeji wetu Oserian Ladies,” alisema nahodha wake, Lydia Akoth.

Thika imebakisha mechi tisa ili kukunja jamvi la mechi za muhula huu ambapo imepangwa kutandaza gozi ya ngombe dhidi ya Kayole Starlets, KGSA, Zetech Sparks, Spedag FC bila kusahau Kisumu All Starlets.

Thika Queens imeundwa na wapigagozi hawa: Awino Phiona (kipa), Ikhumba Lucy, Nury Hadima, Nafula Diana, Sawe Nelly, Akoth Lydia, Wangeci Catherine, Veronica, Wairimu, Mwanahalima ‘Dogo’ Adams, Kapera Nabwire, Rachel Mwema, Halima Regina, Akinyi Gerender, Mkoa Verenetah, Esther Wanjiku, Chepkoech Caroline, Fauzia Omar na Akoth Salome.