Michezo

Thika Queens wajikuta njia panda KWPL

April 10th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

MABINGWA wa zamani katika Ligi Kuu ya Soka la Wanawake ya Kenya (KWPL), Thika Queens wameona giza baada ya kuzimwa kwa mabao 2-0 na Oserian Ladies kwenye mechi iliyochezewa uwanjani Oserian mjini humo.

Naye Quiter Atieno alitikisa wavu mara nne na kusaidia GASPO Women kupiga Makolanders mabao 3-2 pia kunasa bao 1-0 mbele ya Wadadia LG.

Oserian Ladies ilizoa ufanisi huo kupitia Rebecca Akinyi na Margaret Omweri baada ya kila mmoja kupiga moja safi. Matokeo hayo yamefanya GASPO Women kutinga mbili bora kwa alama 16 baada ya kucheza mechi sita. ”Tumepania kuendeleza mtindo huo ili kujiongezea tumaini la kufanya kweli msimu huu,” meneja wa GASPO Women, Edward Githua alisema.

Baadaye Wadadia LG ya kocha, Rishad Sumba ilibeba alama moja ilipotoka sare ya bao 1-1 na Kayole Starlets. Nayo Trans-Nzoia Falcons iliendelea kutembeza vipigo na kuvuna alama sita muhimu ilipokandamiza Mathare United Women kwa mabao 6-2 kisha kuzoa bao 1-0 mbele ya Kayole Starlets. Vihiga Queens imefikisha alama 24 ikiwa kileleni baada ya kupiga mechi nane. Thika Queens imetua saba bora kwa alama 12, moja mbele ya Oserian Ladies.

Wachezaji wa Oserian Ladies (jezi kijani kibichi) kabla ya kuchuana na wenzao hao Vihiga Queens kwenye mechi ya awali ya Ligi Kuu. Vihiga Queens inazidi kutamba inaongoza kwenye jedwali kwa kuzoa alama 24. Picha/ John Kimwere

Trans-Nzioa Falcons iliyomaliza kati ya tano bora msimu uliyopita msimu huu inaonekana inaendelea kushusha ushindi mkali kwenye kampeni hizo. Trans-Nzoia Falcons iliyopandishwa ngazi mwaka 2017 kushiriki kipute hicho ikiwa ndiyo mwaka wa pili tayari imeonekanaa inakuja kwa kishindo huku baadhi ya wachezaji wakiashiria wamepania kushiriki soka ya kimataifa.

Baada ya kucheza mechi za raundi ya sita tayari inaonekana kipute hicho kitaendelea kuzua ushindani mkali baina ya mahasimu wakuu ikiwamo Vihiga Queens, Thika Queens, Oserian Ladies, Trans-Nzoia Falcons, GASPO Women na Soccer Queens inayoendelea kuzinduka.

MATOKEO YA MECHI ZILIZOCHEZWA WIKENDI

Oserian Ladies 2-0 Thika Queens

Mathare United Women 2-6 Trans-Nzoia Falcons

Kibera Girls Soccer 4-0 Vihiga Leeds

Makolanders 2-3 GASPO Women

Soccer Queens 5-0 Eldoret Falcons

Kayole Starlets 1- 1 Wadadia LG

Mathare Unitef Women 0-2 Eldoret Falcons

SPEDAG Ladies 0-2 Vihiga Leeds

Kayole Starlets 0-1 Trans-Nzoia Falcons

GASPO Women 1-0 Wadadia LG