Thika Queens yajinolea CECAFA

Thika Queens yajinolea CECAFA

Na JOHN KIMWERE

LICHA ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kusimamisha Kenya kutoshiriki mechi za kimataifa kwa muda usiojulikana, timu ya wanawake ya Thika Queens inaendelea na mazoezi kujinolea ngarambe ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Thika Queens ya kocha, Benta Achieng ya Ligi Kuu ya Soka la Kenya (KWPL) ilijikatia tiketi ya kushiriki kipute hicho ilipobeba ubingwa wa kipute hicho muhula uliyopita. Meneja wake, Glenston Muganda anasema ”Tunazidi kushiriki mazeozi kujinolea kipute hicho huku tukiwa na imani kuwa FIFA italegeza msimamo wake na kuruhusu Kenya kushiriki mechi za kimataifa.”

Klabu hiyo imepanga kushiriki mechi kadhaa za kupimana nguvu kabla ya kurejelea mechi za ligi wikendi ijayo. Meneja huyo anadokeza kuwa wamepania kushiriki mechi tatu za kirafiki ili kupima uwezo wa wachezaji wao.

Thika Queens ambayo ni mabingwa watetezi imejikuta kwenye wakati mgumu kwenye kampeni za kipute hichi msimu huu. ”Ukweli msimu huu hatuendelei vizuri lakini bado tuna imani tunayo nafasi ya kukaza buti na kuboresha matokeo yetu,” akasema na kuongeza kuwa kampeni za msimu huu kamwe sio mteremko.

Kwenye jedwali la kipute cha KWPL, Thika Queens inashikilia nafasi ya tatu kwa kuzoa alama 20, moja mbele ya Ulinzi Starlets. Thika inajivunia huduma za wachezaji kama:Catherine Githae, Hadima Nuru, Wincate Kinyua, Rebecca Okwaro, Fauzia Omar na Salum Tatu kati ya wengine.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Bethwel Wanjala

Orao: Tuna uwezo kujiondoa mduara hatari

T L