THOMAS OLYBOLE: Kenya ina uwezo wa kuandaa filamu za kiwango cha Hollywood

THOMAS OLYBOLE: Kenya ina uwezo wa kuandaa filamu za kiwango cha Hollywood

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa waigizaji wachache wa kiume wanaoibukia pia wanaopania kuibuka kati ya wanamaigizo mahiri duniani miaka ijayo.

Thomas Obed Olybole ni mwigizaji anayekuja anayefahamika kama jembe la kijiji. Kando na maigizo pia ni mwanamuziki anayeibukia wa nyimbo za Bongo, mwandishi wa filamu pia riwaya za Tamthilia.

”Ingawa kazi zangu hazijapata mashiko ninaamini ninacho kipaji kinachohitaji kupapaliwa zaidi ili kufikia upeo wa kimataifa miaka ijayo,” kijana huyu alisema na kuongeza kuwa anapania kutolegeza kamba licha ya pandashuka zilizoendelea kukabili sekta ya maigizo nchini.

Anasema alivutiwa na masuala ya uigizaji alipotazama kazi zake mwigizaji, David Zependa mzawa wa Mexico. David Zependa anajivunia kushiriki filamu kama ‘Power of destiny,’ na Absimode pasion,’ kati ya zingine.

Alianza kuigiza chini ya kundi la Real Sasa Production mwaka 2004 ingawa baada ya mambo yake kugonga ukuta alikuwa akiwazia kuibuka mwigizaji pia mwanamuziki. Kando na kundi hilo amefanya kazi na makundi mengine kama Zamaradi, Moonbeam, Velglani na Made in Kibera kati ya mengine.

Msanii huyu anajivunia kushiriki filamu kama:’Kina,’ ‘Varshita,’ ‘Shembu,’ ‘Madam Speaker Sir,’ ‘Dunia. Tayari filamu ya ‘Kina’ aliyoshiriki mwaka uliyopita imepata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga ya Maisha Magic Plus na DSTV.

Kijana huyu anasema tangia utotoni mwake alidhamiria kuhitimu kuwa daktari mkubwa ama mwanajeshi lakini anasema haikutimia ambapo aliamua kwa kauli moja kukumbatia masuala ya sanaa.

Anasema Kenya ina tosha kuzalisha filamu za kiwango cha Hollywood kama ilivyo nchini Nigeria lakini inahitaji mshikamano mzuri baina ya wadau wote hasa serikali kuwa mstari wa mbele.

Aidha anadokeza kuwa taifa hili limefurika wasanii chipukizi wanaume na wanawake wanaohitaji kusaidiwa maana wengi wao huache masuala ya uigizaji baada ya kukosa kushikwa mkono pia kukosa wa kuwapa mwelekeo.

”Serikali inastahili kusapoti sanaa ya maigizo bila kulegeza kamba hasa kwa kujenga kumbi za kufanyia kazi ya sanaa kama ilivyo katika mataifa mengine kama Nigeria na Afrika Kusini,” alisema na kuongeza hatua hiyo itawapa motisha zaidi wasanii wanaokuja hasa kuzamia kwenye juhudi za kupalilia talanta zao.

Anasema ndani ya miaka mitano ijayo analenga awe miongoni mwa waigizaji mahiri nchini na duniani akipania kulea wenzake wanaoibukia.

Kama ilivyo kwa wengine msanii huyu anasema kuwa kuwa bado hawajapata mashiko katika sanaa hii wakati mwingi hujipata njiapanda hasa wanaposema hawana hela za kukimu mahitaji muhimu.

”Huwa vigumu kwetu kujitetea kwa marafiki na majirani zetu hasa baada ya kuonekana kwenye runinga kisha kutaja kuwa hatuna fedha,” akasema. Anatoa wito kwa waigizaji wa Kenya wawe wabunifu, wajitume na tuia bidii zaidia bila kuweka katika kaburi la sahau kumtanguliza Mungu kwa kila jambo wanalofanya.

You can share this post!

HARRIET KWAMBOKA: Ipo siku nitatesa katika tasnia ya...

RAEL ODIPO: Uigizaji si mzaha, lazima ujitume