Habari

Tiba ya corona yanukia

June 17th, 2020 2 min read

WANDERI KAMAU na MASHIRIKA

WATAALAMU wa matibabu nchini Uingereza wametangaza kupata dawa ya bei nafuu ambayo inaweza kuua virusi vya corona na kuzuia vifo kwa kiwango cha kutamanisha.

Dawa hiyo inayotumika na mgonjwa kwa njia ya kudungwa inaitwa dexamethasone, na inapatikana kwa urahisi katika mataifa mengi.

Mafanikio ya dawa hiyo yalitokea kama sehemu ya mikakati ambayo imekuwa ikiendeshwa na wataalamu kimataifa kujaribu kupata tiba kamili dhidi ya virusi hivyo.

“Hii ndiyo dawa pekee kwa sasa ambayo imeonekana kupunguza uwezekano wa mgonjwa kufariki kwa kiasi kikubwa. Hii ni hatua kubwa sana,” akaeleza mkuu wa kundi la utafiti, Prof Peter Horby.

Kwa wale wanaosaidiwa kupumua kwa mipira kwa kupewa hewa ya oksijeni wanapoambukizwa virusi vya corona, imebainika dexamethasone inapunguza uwezekano wao wa kufariki kwa asilimia 20.

Kwa wagonjwa waliowekwa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua huwa inapunguza uwezekano wao kufariki kutoka asilimia 40 hadi 28.

Prof Martin Landray, ambaye pia ni mtafiti mkuu, alisema kuwa kati ya wagonjwa wanane waliowekwa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua, kuna uwezekano maisha ya mtu mmoja kuokolewa.

Kulingana na wataalamu, ikiwa dawa hiyo ingetumika kutibu wagonjwa wa corona mara tu baada ya kuripotiwa Uingereza, vifo visivyopungua 5,000 vingeepukika.

Wataalamu wanasema kuwa huenda dawa hiyo ikawafaa sana watu walioambukizwa virusi hasa katika nchi maskini zenye idadi kubwa ya maambukizi.

Humu nchini, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini ilifikia 3,860 jana baada ya visa 133 vipya kuthibitishwa.

Akihutubu kwenye kikao cha kila siku kuhusu hali ya virusi hivyo nchini, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alisema Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa 86, ikifuatwa na Mombasa (27).

Watu 40 pia waliruhisiwa kwenda nyumbani, hilo likifikisha idadi ya wale waliopona kufikia 1,326. Hata hivyo, mtu mmoja zaidi alifariki, hilo likifikisha idadi ya wale walioaga dunia kutokana na virusi nchini kufikia 105.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu watu 19 kati ya 20 walioambukizwa virusi huwa wanapona hata bila kulazwa hospitalini. Na kati ya wale ambao hulazwa, wengi hupona, ijapokuwa baadhi huhitaji oksijeni au mashine maalum za kuwasaidia kupumua. Hao ni miongoni mwa wagonjwa ambao wanalengwa zaidi kufaidika na dawa ya dexamethasone.

Kufikia sasa, dawa hiyo imekuwa ikitumika kupunguza mzio (allergy) na mwasho mwilini.

Utafiti umeonyesha kuwa inaonekana kupunguza madhara ambayo yanaweza kusababishwa mwilini wakati mtu anapoambukizwa virusi vya corona.

Kwenye majaribio yaliyoongozwa na kundi maalum kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, karibu wagonjwa 2,000 waliolazwa hospitalini walipewa dawa hiyo, ikilinganishwa na wengine zaidi ya 4,000 ambao hawakupewa.

“Kuna manufaa makubwa. Matibabu humchukua mtu hadi siku kumi na hugharimu mgonjwa Sh670. Kwa hivyo, inagharimu Sh3,350 kuokoa maisha ya mtu. Ni dawa inayopatikana kote ulimwenguni,” akasema.

Hata hivyo, majaribio yangali yanaendelea ulimwenguni kote kutafuta tiba kamili ya ugonjwa wa Covid-19.

Vile vile, watafiti katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya wangali wanajitahidi kutafuta chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Mojawapo ya chanjo ambazo zimepiga hatua kubwa kufikia sasa inatarajiwa kubainika kama itawezekana kutumiwa ifikapo Oktoba.

Serikali ya Kenya iliamua kuanza kufungua shughuli za kawaida kwa zamu, ambapo jana iliamuliwa hoteli ziongezwe muda wa kuhudumu hadi saa moja unusu usiku.