Tielemans na Maddison wasaidia Leicester kuzamisha chombo cha Brentford ligini

Tielemans na Maddison wasaidia Leicester kuzamisha chombo cha Brentford ligini

Na MASHIRIKA

KIUNGO James Maddison alicheka na nyavu za wapinzani kwa mara ya kwanza tangu Februari mwaka huu na kusaidia Leicester City kupepeta limbukeni Brentford 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Youri Tielemans ambaye ni kiungo mvamizi raia wa Ubelgiji alifungulia Leicester ukurasa wa mabao katika dakika ya 14 kabla ya Mathias Jorgensen kusawazisha mambo katika dakika ya 60. Nusura Brentford wafute juhudi za Tielemans mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila kombora lake likapanguliwa na kipa Kasper Schmeichel.

Bao la pili la Leicester lilizamisha kabisa matumaini ya Brentford baada ya Tielemans kushirikiana vilivyo na Patson Daka na kumwandalia Maddison krosi maridhawa. Ushindi huo wa Leicester uliwapaisha hadi nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 14 sawa na Arsenal, Everton na Manchester United.

Brentford kwa upande wao kwa sasa wanakamata nafasi ya 12 kwa pointi 12 kutokana na mechi tisa za ufunguzi wa muhula huu wa 2021-22.Baada ya mwanzo mbaya zaidi katika kampeni za msimu huu ambapo walipoteza michuano mitatu kati ya sita ya kwanza, Leicester wameanza kuwekea kampeni zao dira.

Ushindi dhidi ya Brentford ulikuwa wao wa tatu mfululizo katika mashindano yote na walishuka dimbani wakiwa na motisha ya kupepeta Manchester United 4-2 katika mechi ya awali ligini kisha kutoka nyuma na kuzamisha Spartak Moscow ya Urusi 4-3 katika Europa League mnamo Alhamisi ya Oktoba 21, 2021.

Huku Leicester wakijinyanyua kama kikosi, wanasoka wao pia wamekuwa wakifufua makali yao katika kiwango cha watu binafsi huku Tielemans kwa sasa akijivunia magoli mawili kutokana na michuano miwili iliyopita.

Bao alilofunga dhidi ya Brentford lilirejesha kumbukumbu za goli la kistadi zaidi alilofunga dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei mwaka huu. Daka aliyepachika wavuni mabao manne dhidi ya Spartak wiki iliyopita aliendeleza ubabe wake ndani ya jezi za Leicester kwa kuchangia bao la pili la waajiri wake dhidi ya Brentford.

You can share this post!

Liverpool wadhalilisha Man-United kwenye EPL ugani Old...

Alaba afunga bao na kusaidia Real Madrid kunyanyasa...

T L