Habari Mseto

Tiger Power afariki akitibiwa hospitalini Embu

January 2nd, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MWANAMUME aliyefahamika kama Tiger Power kwa sababu ya nguvu zake za kiajabu kwa miaka mingi ameaga dunia.

Conrad Njeru Karukenya, alifariki mkesha wa Mwaka Mpya akitibiwa katika hospitali moja katika Kaunti ya Embu.

Kifo cha Tiger Power zilithibitishwa na ndugu yake Ansemoli Kathuri. Kulingana naye, mpenzi huyo wa sanaa alikuwa na umri wa miaka 75 alipoaga dunia katika Hospitali ya Kyeni.

“Alianza kuugua Jumatatu na tulipompeleka hospitali ya misheni ya Kyeni, alifariki akitibiwa,” alisema Kathuri.

Mwanasanaa huyo aliyetoka kijiji cha Kevote Makengi Kaunti ya Embu alishangaza watu kwa nguvu zake za ajabu ambapo angeweza kuvunja misumari kwa meno na kukanyagwa na gari bila kuhisi uchungu.

Hata hivyo, licha ya kutembea maeneo mengi duniani akitumbuiza watu wakiwemo marais, inasikitisha kuwa hakupata malipo ya kuimarisha maisha yake na alikufa akihangaika kama wanasanaa wengine wa miaka ya zamani.

Miaka minne iliyopita alilazimika kuomba msaada wa Sh7,000 kugharamia matibabu yake.

Mnamo 2008 alikabidhiwa tuzo ya Head of States Commendation na Rais mstaafu Mwai Kibaki. Ameacha wake na watoto kadhaa.