Timbe aongoza Buriram kurukia uongozi wa Ligi Kuu Thailand

Timbe aongoza Buriram kurukia uongozi wa Ligi Kuu Thailand

Na GEOFFREY ANENE

WINGA Ayub Timbe Masika ameongoza Buriram United kupepeta wenyeji Chiangmai United na kurukia juu ya jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Thailand, Jumapili.

Masika, ambaye alijiunga na Buriram mnamo Desemba 3 mwaka jana baada ya kuwa bila klabu tangu agure Vissel Kobe mnamo Agosti 11, 2021, alifungua ukurasa wa magoli dakika ya 53.

Supachai Chaided aliongeza mabao mawili yaliyopatikana dakika ya 55 na 60 kabla ya Suphanat Mueanta kuhitimisha ufungaji wa Buriram.

Poonsak Masuk alipachika bao la Chiangmai kufuta machozi dakika ya 71.

Buriram inaongoza ligi hiyo ya klabu 16 kwa alama 35. Bangkok United ni ya pili kwa alama 33, nazo Chonburi, Port na Pathum United zinakamilisha nafasi tano za kwanza kwa alama 29 kila mmoja.

Timu ya Buriram na Bangkok zimesakata mechi 16 kila moja nazo Chonburi, Port na Pathum zimejibwaga uwanjani mara 17. Chiangmai inavuta mkia kwa alama sita baada ya kuandikisha ushindi mmoja, sare tatu na kupigwa mara 12.

You can share this post!

Luis Nani ajiunga na klabu ya Venezia

Mswada walenga kupandisha hadhi lugha ishara

T L