Timbe kutafuta mwanzo mzuri nyumbani Vissel Kobe na Tokushima wakivaana Levain Cup, Dunga huenda pia akachezea Sagan Tosu leo

Timbe kutafuta mwanzo mzuri nyumbani Vissel Kobe na Tokushima wakivaana Levain Cup, Dunga huenda pia akachezea Sagan Tosu leo

Na GEOFFREY ANENE

AYUB Timbe Masika atatumai kuwa na mwanzo mzuri nyumbani klabu yake ya Vissel Kobe itakapoalika Tokushima Vortis katika mechi ya Kundi B ya Kombe la Levain ugani Noevir Stadium Kobe, Jumatano adhuhuri.

Winga huyo wa kimataifa wa Kenya alianza maisha katika klabu yake mpya na mechi ya ugenini ya Ligi Kuu ya J1 League dhidi ya Shonan Bellmare iliyotamatika 0-0 mjini Hiratsuka mnamo Aprili 17.

Licha ya kutopata bao baada ya kutumiwa katika mchuano huo kama mchezaji wa akiba, Masika,28, aliridhisha akisumbua walinzi wa Shonan kwa kasi yake ya kutisha. Huenda akaanzishwa katika mchuano wa leo. Baada ya kutazama mchezaji huyo wa zamani wa Reading FC dhidi ya Shonan, mashabiki wengi wa Vissel Kobe walijitosa kwenye mitandao ya kijamii wakisema wanasubiri kwa hamu kubwa kumuona akisakata kabumbu ugani Noevir.

Mabingwa watetezi FC Tokyo wanaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kupepeta Tokushima 1-0 mnamo Machi 3 na Vissel 2-0 Machi 28.

Vissel itajibwaga uwanjani mwake ikiwa na alama tatu katika kipute hiki kutokana na ushindi wake wa magoli 3-1 dhidi ya Oita Trinita 3-1 katika mechi ya ufunguzi mnamo Machi 2.

Vijana hao wa kocha Atsuhiro Miura wako mbele ya Oita kwa tofauti ya ubora wa magoli. Oita ilikung’uta Tokushima 1-0 mnamo Machi 27. Tokushima inavuta mkia bila pointi.

Jumatano pia itakuwa zamu ya Sagan Tosu inayoajiri mshambuliaji Mkenya Ismael Dunga kualika Avispa Fukuoka. Vijana wa kocha Kim Myung-hwi hawana alama baada ya kupoteza mechi zao mbili za kwanza za Kundi A dhidi ya Kashima Antlers 3-0 (Machi 3) na Hokkaido Consadole Sapporo 5-1 (Machi 27). Dunga, 28, ambaye alikuwa mali ya klabu ya Vllaznia nchini Albania mwaka 2020, alianza mazoezi yake Aprili 15 baada ya kukamilisha karantini ya lazima nchini Japan.

  • Tags

You can share this post!

IEBC: Mchakato wa kuteua makamishna 4 wapya kushika kasi...

Malalamiko ya MCK kwa DCI