Timo Werner arejea kambini mwa RB Leipzig baada ya kuagana na Chelsea

Timo Werner arejea kambini mwa RB Leipzig baada ya kuagana na Chelsea

Na MASHIRIKA

RB Leipzig wamemsajili upya fowadi Timo Werner kutoka Chelsea, miaka miwili baada ya sogora huyo raia wa Ujerumani kutua ugani Stamford Bridge.

Chelsea walioweka mezani kima cha Sh6.4 bilioni kwa ajili ya Werner mnamo 2020, sasa wamemwachilia kurejea Leipzig kwa mkataba wa miaka minne uliogharimu Sh3.6 bilioni pekee.

“Nina furaha kurejea Leipzig ambao sasa nitawachezea hadi 2026. Najihisi nyumbani kabisa kwa kuwa hiki ni kikosi nilichowahi kukichezea kati ya 2016 na 2020,” akasema Werner, 26.

Werner alifungia Chelsea mabao 23 kutokana na mechi 89 katika mashindano yote huku akisaidia miamba hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuzoa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021.

Alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wakihemewa pakubwa na vikosi maarufu vya bara Ulaya mnamo 2020 na akahiari kujiunga na Chelsea baada ya kutupilia mbali ofa za kusajiliwa na Liverpool, Bayern Munich na Atletico Madrid.

Alipachika wavuni mabao 95 kutokana na mechi 159 akivalia jezi za Leipzig katika awamu ya kwanza kambini mwa kikosi hicho kilichomsajili kutoka Stuttgart mnamo 2016.

Hata hivyo, makali yake yalishuka baada ya kuhamia Chelsea ambako alifunga mabao 10 pekee katika kipindi cha misimu miwili.

Leipzig pia wamemsajili fowadi raia wa Slovenia, Benjamin Sesko, 19, ambaye atasalia kambini mwa Red Bull Salzburg kwa mkopo hadi Julai 2023 kabla ya kutia saini mkataba wa miaka mitano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Benzema aongoza Real Madrid kukomoa Eintracht Frankfurt na...

Wakazi wa Bondo wakesha wakisubiri matokeo ya urais

T L