Michezo

Timu 12 tayari kuwania ubingwa kombe la wanawake la raga

October 11th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU zote 12 zitakazoshiriki Kombe la Wanawake la raga ya wachezaji saba kila upande mnamo Oktoba 12-13 nchini Tunisia ziko tayari kuwania ubingwa.

Mshindi wa kombe hili ataingia michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Taarifa kutoka nchini Tunisia zimesema Ijumaa kuwa washiriki wote wakiwemo mabingwa watetezi Kenya, wako tayari mjini Monastir na hata kufanya mazoezi.

Lionesses ya Kenya ilizaba Senegal 41-0 na Madagascar 42-0 katika mechi za makundi, ikalemea Zambia 42-5 katika robo-fainali, Madagascar 27-0 katika nusu-fainali na Uganda 29-7 katika fainali mwaka 2018 jijini Gaborone nchini Botswana.

Taji hili lilikuwa la kwanza kabisa la Kenya baada ya kumaliza ya pili nyuma ya Tunisia mwaka 2012 mjini Tunis na pia nyuma ya Afrika Kusini mwaka 2014 (Machakos), 2015 (Afrika Kusini), 2016 (Zimbabwe) na 2017 (Monastir).

Kenya, ambayo ilishiriki Olimpiki mwaka 2016 baada ya kuchukua nafasi ya Afrika Kusini iliyojiondoa, itaanza kampeni yake dhidi ya Ghana na kukamilisha mechi za Kundi A dhidi ya Senegal.

Bingwa wa Afrika ataungana na Japan (wenyeji), na New Zealand, Amerika, Canada na Australia zilizomaliza Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 katika nafasi nne za kwanza katika Olimpiki.

Brazil pamoja Uingereza, ambao walishinda mashindano ya Amerika Kusini na Bara Ulaya mtawalia, pia wameshafuzu kushiriki Olimpiki. Maeneo ya Oceania na Asia yataandaa mashindano yao ya kuchagua wawakilishi wao mwezi Novemba. Mashindano ya kuchagua timu mbili za mwisho zitakazoshiriki Olimpiki yataandaliwa Juni mwaka 2020.

Makundi ya Kombe la Afrika (2019):

A – Kenya, Senegal, Botswana, Ghana

B – Uganda, Zimbabwe, Afrika Kusini, Zambia

C – Tunisia, Madagascar, Morocco, Mauritius