Michezo

Timu 'B' ya Chelsea yapiga Krasnodar na kusonga mbele UEFA wakiwa kileleni mwa Kundi E

December 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO Jorginho alifungia Chelsea bao la penalti katika dakika ya 28 na kusaidia waajiri wake hao kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Krasnodar katika mchuano wa Kundi E kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 8, 2020.

Kocha Frank Lampard alifanyia kikosi chake cha Chelsea kilichowapiga Leeds United 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 5 mabadiliko 10.

Mkufunzi huyo raia wa Uingereza alimwajibisha chipukizi Tino Anjorin kwa mara ya kwanza huku kiungo Billy Gilmour, 19, akichezeshwa pia kwa mara ya kwanza tangu apone jeraha la goti lililomweka mkekani kwa kipindi kirefu.

Licha ya wachezaji wa timu ‘B’ ya Chelsea kutamalaki mchezo katika dakika za mwanzo, nyavu zao zilitikiswa katika dakika ya 24 kupitia kwa Remy Cabella aliyemwacha hoi kipa Kepa Arrizabalaga.

Chelsea walisawazisha dakika nne baadaye kupitia kwa Jorginho aliyefunga penalti iliyotokana na tukio la fowadi Tammy Abraham kuchezewa visivyo na kiungo Kaio ambaye ni raia wa Brazil.

Matokeo hayo yalihakikisha kwamba Chelsea wanakamilisha kampeni za makundi kileleni mwa Kundi E kwa alama 14 kutokana na mechi sita. Sevilla walifuzu pia kwa hatua ya mwondoano baada ya kumaliza kampeni za Kundi E katika nafasi ya pili kwa alama 13 baada ya kupiga Rennes 3-1.

Ni matarjio ya kocha Lampard kwamba ushindi huo utawapa sasa vijana wake hamasa zaidi ya kupepeta Everton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayowakutanisha na Everton mnamo Disemba 12, 2020 uwanjani Goodison Park.