Michezo

Timu ya handiboli yaelekea Rwanda kusaka ubingwa wa Afrika

August 7th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya handiboli ya Kenya ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 iliondoka nchini Agosti 6 saa mbili usiku kuelekea nchini Rwanda kwa mashindano ya Afrika.

Mabingwa hawa wa Afrika Mashariki (Ukanda wa Tano) watatumia basi kutoka Kimilili katika kaunti ya Bungoma kupitia kaunti ya Busia na miji kadhaa nchini Uganda kabla ya kuwasili nchini Rwanda. Imeratibiwa kuwasili jijini Kigali saa saba mchana Agosti 7.

Timu ya Kenya, ambayo ililemea Ethiopia 22-17 katika fainali ya Ukanda wa Tano jijini Kampala nchini Uganda mnamo Mei, itaanza kampeni ya kutafuta tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia dhidi ya mabingwa wa Ukanda wa Tatu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mnamo Agosti 9 uwanjani Amahoro jijini Kigali.

Wakenya wako katika Kundi A. Mbali na DR Congo, vijana wa kocha Gerald Juma watalimana na mabingwa wa Ukanda wa Pili Zambia mnamo Agosti 10.

Timu ya Kenya imekuwa ikifanyia mazoezi yake katika Shule ya Upili ya Kimilil Boys. Mabingwa hawa wa Kenya wamechangia wachezaji wanane ambao ni Chris Muluki, Edwin Wasilwa, Jimmy Wenani, Duncan Kimutai, Lewis Kiptoo, Elias Khisa, Joseph Simiyu na Douglas Wekesa.

Alphonse Wanzala, Samson Hope na Daniel Okinyi wanatoka Shule ya Upili ya Kanyawanga kutoka kaunti ya Migori, Bonface Kiplimo na Stephasus Koech kutoka Kitany Boys kaunti ya Uasin Gishu naye Simon Bosire ni mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Mukumu katika kaunti ya Kakamega. Kundi B linaleta pamoja Nigeria, Cameroon na Guinea.