Michezo

Timu ya Kenya ya mbio za nyika yapokelewa kishujaa kutoka Denmark

April 1st, 2019 2 min read

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

Timu ya Kenya ilipokelewa kishujaa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya kuwasili kutoka mjini Aarhus nchini Denmark mnamo Jumatatu saa nane mchana.

Kama kawaida, ilikuwa nyimbo na densi pamoja na unywaji cha maziwa ya kitamaduni ya Kikalenjin ya mursik.

Baadhi ya viongozi waliowasili JKIA kulaki wanariadha hao ni Gavana wa kaunti ya Kericho Paul Chepkwony, Mbunge wa Kepkelion East, Joseph Limo na kaimu kamishna Japson Gitonga, ambaye alikuwa afisa wa pekee kutoka serikali kuu aliyefika katika uwanja huo.

Bingwa wa mbio za nyika za watu wazima za wanawake (kilomita nane) Hellen Obiri na mshindi wa mbio za nyika za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 (kilomita sita) Beatrice Chebet ndio walioongoza timu ya Kenya kurejea nyumbani.

Mfalme wa mbio za kilomita 21 duniani Geoffrey Kamworor, ambaye alipokonywa taji la dunia la mbio za nyika za watu wazima za wanaume na Mganda Joshua Cheptegei, aliwasili nchini Machi 31.

Meneja wa timu ya Kenya, Benjamin Njoga na kocha mkuu David Letting’ walisema kwamba matokeo yangekuwa bora zaidi baada ya kujifunza mengi kutoka nchini Denmark.

“Tungefanya bora zaidi, lakini funzo kubwa tumepata kutoka Denmark ni kwamba tungetuma kikosi mapema kuangalia sehemu ya mashindano ambayo ilikuwa ngumu,” alisema Njoga. “Maandalizi yetu hayakugusia mazoezi ya sehemu iliyojaa milima kama tuliyopata mjini Aarhus ambayo ilikuwa ngumu sana.”

Njoga alisema kwamba Kenya itatilia maanani katika sehemu zote za mazoezi pamoja na mahasimu wao katika mashindano ya siku za usoni.

Aidha, alisema kwamba taifa la Kenya linastahili kupongeza ujasiri ulioonyeshwa na wanariadha wake licha ya changamoto ambazo hawakutarajia kupata, hasa sehemu ya mashindano.

Letting alisema kwamba kikosi chake kilikuwa na shinikizo la kutetea taji kwa sababu kila timu ililenga kuvua Wakenya ubingwa.

Alifichua kwamba mahasimu wao wakuu Ethiopia na Uganda walizuru eneo la mashindano mwezi Oktoba mwaka 2018 kuangalia sehemu hiyo. “Ethiopia na Uganda pia walifika nchini Denmark mapema sana kwa mashindano. Hiyo ndio sababu walikuwa hatua moja mbele yetu katika matayarisho kutuliko,” alisema.

Naibu kocha Julius Kirwa alisema ufanisi waliopata mazoezini haukuwasidia kwa sababu walisafiri kwa saa 18 na kufika Denmark siku moja kabla ya mashindano.

“Tulifika Alhamisi na kupata kuona sehemu ya mashindano usiku wa kuamkia mashindano,” alisema Kirwa. “Tulikuwa na wanariadha waliokuwa wamefura miguu kwa sababu ya safari ndefu.”

Kirwa alisema kwamba kukaa mjini Dubai kwa karibu saa nzima kusubiri ndege nyingine ya kuelekea Denmark haikuwa njia nzuri ya timu kusafiri.

Naibu Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Paul Mutwii alishambulia serikali akiitaka ijifunze kupeana tiketi za ndege mapema. “Pia tunahitaji kutumia ndege zinazofaa ili timu iweze kupata matokeo mazuri,”alisema Mutwii.

Obiri, ambaye alilakiwa na mumewe na meneja Simon Nyaudi na mtoto wao wa kike Tania, alishukuru Wakenya kwa usaidizi wao mkubwa. “Naahidi ushindi pia katika Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar mwezi Oktoba mwaka huu,” alisema Obiri, ambaye atakuwa akitetea taji lake la mbio za mita 5,000.

Chebet, ambaye alipokelewa na kocha wake Paul Kemei na wazazi wake Francis na Lilian Kirui, alisema kwamba sasa anaelekeza macho yake kwa mashindano ya Bara Afrika ya Under-20 yatakayofanyika nchini Ivory Coast baadaye mwezi huu.