Michezo

Timu ya kitaifa ya Karate kuteuliwa mwishoni mwa wiki hii

March 7th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO
MASHINDANO ya Karate ya Kenya Opens yanatarajiwa kuendelea katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya kati ya Machi  9 na Machi 10, 2019.
Katibu mpanga ratiba wa mashindano hayo Gabriel Mutuku, alitoa masharti kwa washiriki wa mchezo huo huku kila mchezaji akitakiwa kufika ukumbini saa mbili kamili za asubuhi.
Baadhi ya matakwa wanayostahili kutimiza kabla ya kuruhusiwa kushiriki ni kubeba vifaa vya kuchezea bila kusahau sare.
Mchezaji yeyote atalazimika kubeba vifaa vya kujikinga, glavu za mchezo, kifaa cha mdomoni (Mouth Guard), na kifaa cha mguuni.
Mchezo huo utashirikisha wasichana na wavulana huku wakicheza mbinu za Kata na Kumite.
Alisema orodha kamili ya wachezaji itapangwa mnamo Machi 8, 2019.
Kuondolewa
Mchezaji yeyote atakayefika akiwa amechelewa kujisajili ataondolewa kwenye orodha hiyo.
Alisema mashindano hayo yatakuwa ya kujipanga katika michezo kadha ya kimataifa itakayofanyika mwaka huu wa 2019.
Baadhi ya mashindano hayo ni Africa Beach Games ambayo ni mchezo wa Kata utakaofanyika mji wa Sal, Cape Verde.
Mashindano mengine ni yale ya Zone 5 ANOCA Youth Games yatakayoandaliwa jijini Kigali, Rwanda.
Kuna mchezo wa UFAK ya watu wazima na Wale wadogo itakayofanyika Gaborrone, Botswana.
Kuna mchezo wa All Africa Games ya Rabat, Morocco. Halafu kuna ile ya kujiandaa kwa Olimpiki za mwaka wa 2020.
Vigezo
Alisema mashindano hayo yamepangwa kulingana na uzani na mchezo wanaowakilisha.
Kiwango cha Cadets miaka 14-15 wavulana na wasichana watashiriki Kata na Kumite.
Kuna Junior kati ya miaka 16-17 kwa wasichana na wavulana. Pia kuna Novices. Wale wa umri wa miaka 18 na zaidi watashiriki Kumite na Kata.
Wakufunzi wote kutoka Kaunti tofauti wameombwa kuwasajili na kuwasilisha majina ya wachezaji mapema ili kuwe na kazi rahisi ya kupanga ratiba kamili jinsi watakavyocheza.