MichezoVideo

Timu ya Riadha ya Kenya yapokelewa kishujaa JKIA

March 19th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya riadha ya Kenya Jumatatu imepokelewa kishujaa kutoka nchini Algeria ambako ilishinda ubingwa wa Afrika baada ya kuzoa medali tatu za dhahabu, nne za fedha na moja ya shaba kwenye Mbio za Nyika za Afrika za mwaka 2018.

Mabingwa wa mbio za nyika za Afrika, Kenya, wakaribishwa kwa nyimbo na densi uwanjani JKIA Machi 19, 2018. Picha/ Geoffrey Anene

Vijana hao kocha John Kimetto walitumbuizwa kwa nyimbo za kitamaduni walipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kabla ya kuelekea katika hoteli ya kifahari ya Weston kwa chakula cha mchana baada ya mahojiano na wanahabari.

Timu nzima ikiongozwa na Kimetto ilimshukuru Mungu kwa kuiwezesha kutwaa ubingwa. Kimetto alisema ameridhishwa na matokeo ya wanariadha wake.

Kutoka kushoto: Kocha John Kimetto, Naibu wa meneja wa timu Duncan Ogare, bingwa wa zamani wa marathon duniani Catherine Ndereba na Celliphine Chespol wakipiga picha katika uwanja wa ndege wa JKIA. Picha/ Geoffrey Anene

“Nafurahi tulipigania kila medali katika vitengo vyote. Ingawa tulilenga kuzoa medali zote, nimeridhika na kazi yetu hasa kwa sababu sehemu ya mashindano ilikuwa telezi sana,” alisema.

“Wakimbiaji wangu walifuata maagizo yangu. Hata (Celliphine) Chespol, ambaye alianza kusherekea mapema kabla ya kugundua hajakamilisha mzunguko mmoja, alisikia maagizo na akajikaza na kuibuka mshindi,” alifichua.

Mabingwa wa mbio za nyika za Afrika, Kenya, wakaribishwa kwa nyimbo na densi uwanjani JKIA Machi 19, 2018. Picha/ Geoffrey Anene

Shirikisho la Riadha nchini (AK) pia limefurahishwa na matokeo haya.

Rais wa AK Jackson Tuwei ameambia wanahabari kwamba, “Timu ilipata matokeo ya kupendeza sana. Licha ya kupoteza taji la binafsi katika mbio za kilomita sita za wanawake, nafurahi tulishinda taji la timu katika kitengo hiki baada ya muda mrefu sana.”

Kenya ilizoa medali tatu za dhahabu kupitia Celliphine Chespol (kilomita 10 wanawake), Alfred Barkach (kilomita 10 wanaume) na Ronex Kipruto (kilomita nane wanaume).

Ilishinda nishani za fedha kupitia Margaret Chelimo (kilomita 10 wanawake), Julius Kogo (kilomita 10 wanaume) na Stanley Waithaka (kilomita nane wanawaume) na pia timu ya mbio za mseto za kupokezana vijiti. Hellen Ekalale alishindia Kenya medali ya shaba katika mbio za kilomita sita wanawake.

Mabingwa wa mbio za nyika za Afrika, Kenya, wakaribishwa kwa nyimbo na densi uwanjani JKIA Machi 19, 2018. Picha/ Geoffrey Anene

Mbali na mataji hayo ya binafsi, Kenya pia ilishinda mataji ya timu katika vitengo vinne.

Tuwei alionya kwamba Kenya inastahili kuweka mikakati bora kuhakikisha inasalia miamba wa mbio za nyika baada ya kushuhudia ushindani mkali ukitoka kwa Waganda Jumamosi iliyopita.

Aidha, Tuwei amefichua kwamba wanamedali Chespol, Barkach, Kipruto, Waithaka, Chelimo, Kogo na Ekalale watajumuishwa katika timu itakayopeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Australia mwezi Aprili.

“Tutanataka pia kuwaona mkihudhuria mbio za uwanjani tutakapochagua kikosi kitakachowakilisha Kenya katika Riadha za Dunia za Under-20 zitakazofanyika nchini Finland mnamo Julai 10-15 2018.

Video Gallery