Timu ya tenisi ya meza ya Kenya yaingia Qatar kwa mchujo wa Olimpiki

Timu ya tenisi ya meza ya Kenya yaingia Qatar kwa mchujo wa Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya tenisi ya meza ya Kenya inatarajiwa kupigania tiketi za kushiriki Michezo ya Olimpiki kwenye mchujo wa kimataifa utakaoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo Machi 11-18.

Wanatenisi hao wanne walipokea mavazi rasmi ya timu ya Kenya kutoka kwa maafisa wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Eliud Kariuki na Winnie Kamau katika taasisi ya Goan ambako wamekuwa wakifanyia mazoezi tangu mwezi Februari.

Wachezaji watakawakilisha Kenya jijini Doha kwenye tenisi hiyo ya kuchezewa juu ya meza ni Brian Mutua, Josiah Wandera, Doreen Juma na Lydia Setey.

Kiongozi wa msafara ni James Oronge nao Anthony Ringui na Mohammed Salat ni makocha. Kamau pia yuko katika timu hiyo ya Kenya kuwakilisha NOC-K katika kuichanganua na kuona inavyoendelea na safari yake ya kufuzu kushiriki Olimpiki.

“Tunaenda kukutana na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kwa hivyo tunatarajia ushindani mkali,” alisema Wandera. Timu hiyo iliratibiwa kuelekea Doha mnamo Jumatano usiku. Imepata ufadhili kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya michezo na NOC-K.

You can share this post!

Liverpool wazamisha RB Leipzig na kujikatia tiketi ya...

Kenya yaandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya...