Michezo

Timu za EPL zakubaliwa kuchezesha wachezi 5 wa akiba

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) sasa watakuwa na uwezo wa kuchezesha hadi wachezaji watano wa akiba, badala ya watatu, katika mchuano hadi mwishoni mwa msimu huu.

Hii ni baada ya pendekezo hilo kuidhinishwa na washiriki wote wa kipute hicho kitakachorejelewa mnamo Juni 17, 2020.

Klabu kwa sasa itakuwa na fursa ya kupanga wachezaji tisa katika vikosi vya akiba badala ya saba waliozoeleka.

Mawakili wa klabu za EPL waliwawasilishia wasimamizi wa soka ya Uingereza pendekezo la kuwajibishwa kwa hadi wachezaji watano wa akiba katika mchuano mnamo Aprili 27, 2020 wakidai kwamba hatua hiyo itapunguza visa vingi vya majeraha miongoni mwa masogora.

Tangazo la raundi chache za kwanza tangu kusitishwa kwa kampeni za EPL kwa sababu ya corona mnamo Machi 13, 2020 linatarajiwa kutolewa Juni 5, 2020.

Vinara wa EPL walikuwa wepesi wa kuidhinisha pendekezo hilo kwa kuwa ni suala lililowahi kujadiliwa kwa kina na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa pamoja na Bodi ya Kimataifa ya Mashirikisho ya Soka (IFAB) na kuafikiwa kuwa mojawapo ya njia kuu zinazoashiria kwamba maslahi ya wachezaji yanazingatiwa ipasavyo.

Kati ya wachezaji wote watano wa akiba, ni watatu pekee watakaokubaliwa kuingia uwanjani katika nyakati tofauti tofauti za mchezo isipokuwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Mchezaji wa sita wa akiba huenda akaruhusiwa kuwajibishwa uwanjani wakati wa kipindi cha ziada; yaani baada ya muda wa dakika 90 za kawaida za mchezo kukamilika na mechi kuingia katika dakika 30 za ziada.

Kanuni hii mpya kuhusu wachezaji wa akiba, itatekelezwa pia katika kiwango cha timu za taifa kwa mechi zitakazokuwa zimeratibiwa kusakatwa hadi Disemba 31, 2021.