Michezo

Timu zaanza kujiandaa kwa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu

November 15th, 2020 2 min read

NA JOHN KIMWERE

INGAWA janga la corona lilichangia shughuli za michezo kusitishwa kote nchini, timu za soka la wanawake zimeanza kupiga hesabu ya jinsi zitakavyoshusha ushindani wa kufa mtu kwenye mbio za Ligi Kuu (KWPL) muhula huu.

Kampeni za kipute cha msimu huu zitajumuisha jumla ya vikosi 16 zikiwamo klabu tatu mpya zilizopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza. Timu hizo ni Ulinzi Starlets, SEP Girls na Nakuru West Queens.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wiki iliyopita lilitoa ratiba ya ngarambe hiyo ambapo imepangwa kukunjua jamvi mwishoni mwa Novemba 2020 na kumaliza Mei 2021.

MAKUNDI MAWILI

Ni wazi kwamba wachezaji wa vikosi hivyo wanapaswa kushiriki mazoezi kujiandalia kampeni hizo ingawa serikali bado haijaruhusu mikusanyiko ya watu. Katika mpango mzima viongozi wa klabu hizo wanasema hawana budi kuanza mazoezi huku wakifuata masharti yaliyotangazwa na serikali kwenye juhudi za kuzuia msambao wa virusi vya corona. Timu zitakaoshiriki mechi za msimu huu kwa mara nyingine zimegawanywa katika makundi mawili Kundi A na B.

”Ingawa katika klabu yangu hamna mchezaji ameambukizwa ugonjwa wa covid 19 tayari unatatiza maandalizi yetu maana wachezaji wanahofia kujikuta pabaya,” kocha wa Makolanders, Rishadi Shedu alisema na kuongeza kwamba wamelazimika kuzungumza na wakuu wa kituo cha polisi katika eneo lao ili kuanza kupiga tizi kujiweka vizuri kuanza kampeni zao.

VIHIGA QUEENS

Mapema mwaka huu Shedu aliteuliwa kuongoza Makolanders ambapo amepania kutumia tajriba ya muda mrefu kuhakikisha kikosi hicho kinaibuka kati ya nafasi bora katika kampeni za muhula huu. Shedu anajivunia kufunza timu kadhaa zilizokuwa zikishiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) miaka iliyopita.

Warembo wa Thika Queens kati ya timu zinazojivunia kubeba ubingwa huo mara tatu wanalenga kujituma mithili ya mchwa kukabili wapinzani wao kwenye mechi za msimu huu. Pia Vihiga Queens inajivunia kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo inalenga kuendeleza ubabe wake kwenye jitihada za kutetea kombe hilo.

Katika mpango mzima kocha wa klabu matata wakiwamo Joseph Wambua Mwanza (Ulinzi Starlets), Alex Alumira (Vihiga Queens) pia Edward Githua meneja (Gaspo Womens) na Fredrick Chege ofisa mkuu (Thika Queens) wanakiri kwamba kipute cha msimu mpya kitashuhudia ushindani mkali.

”Bila kujipigia debe sina shaka kutaja kuwa msimu kitanuka maana tunalenga kufanya kweli licha ya kuwa ndio mwanzo wa ngoma tunashiriki kampeni za ligi kuu,” kocha wa Ulinzi Starlets aliambia mwanaspoti. Hata hivyo anatoa wito kwa serikali ifanye juhudi kwenye jitihada za kupaisha soka la wanawake nchini.

Kundi A: Linashirikisha: Ulinzi Starlets, Makolanders, Gaspo Womens, Kayole Starlets, Zetech Sparks, Mathare United Women, Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) na Thika Queens. Kundi B: Linajumuisha: Trans Nzoia Falcons, Vihiga Queens, Oserian Ladies, Kisumu AllStarlets, Eldoret Falcons, Wadadia LG, SEP Girls na Nakuru West Queens.