Habari MsetoSiasa

Timua wanaotatiza juhudi za kukabili ufisadi, Uhuru aambiwa

March 19th, 2019 2 min read

Na BARNABAS BII

VIONGOZI kadhaa wa Rift Valley Jumatatu walitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta aadhibu wanachama wa Jubilee wanaotatiza juhudi za kupambana na ufisadi.

Kulingana nao, viongozi aina hiyo wanaweka hatarini sifa itakayoachwa na Rais wakati atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi mwaka wa 2022.

Walipuuzilia mbali madai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga viongozi wa eneo moja, wakamtetea Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti kwa kukamata washukiwa wa ufisadi.

Viongozi kutoka Chama cha Jubilee, vyama vya upinzani na wa kijamii walikashifu vikali wandani wa Naibu Rais William Ruto kwa madai yao kwamba Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), inatumiwa kuhujumu miradi mikubwa ya Jubilee kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

“Inafedhehesha kwa kiongozi ambaye yuko ndani ya serikali kuzungumza kinyume na Rais Kenyatta ambaye amekuwa akisema wazi mara kwa mara kwamba ana imani kwa DCI na asasi nyingine za kitaifa kupambana na ufisadi,” akasema Bw Paul Kibet, ambaye ni mratibu wa Chama cha KANU katika eneo la Rift Valley.

Alitoa wito kwa asasi husika zizidishe juhudi zao katika vita dhidi ya ufisadi na kurudisha mali zilizoibwa huku wakichukua hatua za kisheria dhidi ya washukiwa wa ufisadi bila kujali nafasi zao katika jamii.

Naibu Rais na wandani wake wamekuwa wakidai Bw Kinoti anatumiwa kuhujumu miradi ya Jubilee kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

Lakini Mbunge wa Cherang’any, Bw Joshua Kutuny alimuonya Dkt Ruto na wandani wake dhidi ya kutumia jamii nzima kutetea misimamo yao na vile vile kutishia jamii nyingine.

Alionya pia dhidi ya kutusi afisi ya rais katika vita dhidi ya ufisadi.

Katibu Mkuu wa KANU, Bw Nick Salat alisema wanasiasa hawawezi kukubaliwa kumshambulia Rais kwa maneno kwani haifai kuashiria kwamba kiongozi wa taifa anaagiza jinsi uchunguzi ufanywe kwa sakata mbalimbali zilizofichuliwa majuzi.

“Ninataka kuambia hawa wanasiasa wanaojidai kuzungumza kwa niaba ya Wakalenjin waachane na sisi. Vita dhidi ya ufisadi havifai kuchukuliwa vya kibinafsi jinsi wanavyofanya. Inasikitisha wanaingiza jamii nzima katika suala hili. Hili ni jambo ambalo hatutalikubali kamwe,” akasema Bw Salat.

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter alisema watu waliohusishwa na ufisadi wanafaa wajiandae kubeba misalaba yao wenyewe bila kuingiza jamii nzima kwa biashara zao haramu.

Hii ni baada ya Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang na wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Caleb Kositany (Soy) kumwambia Rais awaeleze sababu halisi kuhusu kwa nini anampiga vita naibu wake.

Viongozi hao waliozungumza wiki iliyopita katika mazishi iliyofanywa eneo la Ziwa, Kaunti ya Uasin Gishu walimlaumu Rais kwa kutumia mwafaka kati yake ya Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuadhibu watumishi wa umma ambao ni wa jamii ya Wakalenjin na kuzuia utekelezaji wa miradi mikubwa katika eneo hilo.

Mnamo Jumapili, viongozi wengine ambao ni pamoja na mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko pia walijitokeza kuwashtumu wenzao wa Rift Valley kudai kuwa wanalengwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Bi Mboko hasa alimtaka Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen ajitokeze kuelezea anachofahamu kuhusu kashfa ya mabwawa na sio kutoa madai tu.