Kimataifa

Tineja ajuta baada ya kuuza figo anunue iPhone na iPad

January 10th, 2019 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

WATU watano walishtakiwa katika mahakama moja China kwa kumjeruhi kijana mmoja kimakusudi, alipoamua kuuza figo yake kwa Sh2 milioni ili apate pesa za kununua simu ya iPhone na tableti ya iPad.

Walioshtakiwa wanahusisha daktari wa upasuaji kutoka eneo la China Kusini ambaye alimtoa figo kijana huyo wa miaka 17.

Viongozi wa mashtaka jiji la Chenzhou, mkoa wa Hunan walisema kuwa mmoja wa washtakiwa alipokea pesa hizo ili kupanga namna kijana huyo angetolewa figo yake.

Hata hivyo, kijana huyo aliyefahamika kwa jina Wang alilipwa Sh200,000 pekee baada ya kutolewa kiungo hicho cha mwili, huku zilizosalia zikigawanywa kati ya daktari na aliyepanga mpango huo.

Tineja huyo anadaiwa kutoka mkoa wa Anhui ambapo kuna ukosefu mkubwa wa kazi na sasa anaugua kutokana na upasuaji huo ambao haukuenda ipasavyo.

Hata hivyo, baada ya kufanyiwa upasuaji huo Aprili mwaka jana, Wang aliweza kununua iPhone na iPad. Mamake alipomuuliza alivyoweza kununua vifaa hivyo, tineja alikiri kuwa aliuza figo yake.

Hata hivyo, haijafamika nani alipokea na kulipia figo hiyo. Biashara ya viungo vya mwili imeshika kasi China huku habari zake zikijaa mitandaoni.

Habari za serikali zinaonyesha kuwa Zaidi ya watu milioni moja huhitaji kubadilishiwa viungo vya mwili kila mwaka katika taifa hilo, japo chini ya asilimia moja huweza kupata, jambo ambalo limefanya soko la viungo kushika kasi.

Vilevile, Wachina wachache hukubali viungo vyao kutumiwa kusaidia wagonjwa baada yao kufa, hali ambayo imefanya soko haramu la viungo kuzidi.

China ilipiga marufuku biashara ya viungo vya mwili 2007, ikiweka sharia kuwa anayetaka kumsaidia mtu afanye hivyo bila malipo na kwa hiari yake.

Bidhaa za apple zina umaarufu katika taifa hilo, lakini bei yake iko juu ikilinganishwa na uwezo wa raia wengi wa taifa hilo. Bidhaa za iPhone huanzia Sh40,000 kwenda juu na iPad huanzia Sh19, 000.

Lakini sasa hali ya kijana huyo y kiafya imezidi kudhoofika, wakasema viongozi wa mashtaka. Washukiwa Zaidi wa kisa hicho wanazidi kuchunguzwa.