Kimataifa

Tineja motoni kwa kuruka ua adandie ndege ikipaa

July 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

ATLANTA, AMERIKA

MWANAMUME alikamatwa na polisi alipojaribu kudandia ndege iliyokuwa ikiondoka katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Hartsfield-Jackson ulio Atlanta, Amerika

Ilisemekana mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Jhryin Jones, 19, aliingia uwanjani humo kwa kuruka ua.

Alielekea moja kwa moja hadi katika barabara ya ndege na kudandia ubawa wa ndege, kisha akaanza kubisha hodi dirishani.

Video iliyosambazwa mitandaoni ambayo inaaminika ilinaswa na mmoja wa wasafiri waliokuwa ndani ya ndege, ilimwonyesha mwanamume huyo akiwa amevaa chupi huku akishikilia kitu kilichoonekana kama nguo mkononi mwake.

Ilikuwa ni kama sinema uwanjani kwani ilibidi maafisa wa usalama waharakishe kufuata ndege hiyo kwa magari kadhaa yaliyokuwa na ving’ora.

Polisi walifanikiwa kumkamata, wakanukuliwa kwenye vyombo vya habari wakisema kuwa alishtakiwa baadaye kwa kuingia uwanja wa ndege bila kibali, kuonyesha uchi wake hadharani na kujaribu kukwepa sheria kwa kutoroka polisi.

-Imekusanywa na Valentine Obara