Habari

UTAMADUNI: Eneo ambako kina baba na watoto hutengewa titi kunyonya

April 1st, 2018 3 min read

Na SHABAN MAKOKHA

Kwa ufupi:

  • Wanaume wa Butere wafichua kwamba wao hunyonya matiti za wake zao ili kuondoa mikosi na kuzuia kuyeyuka kwa ashiki za mapenzi za mama baada ya kuzaa, ambapo baba na mtoto kila mmoja hutengewa titi lake
  • Wametetea vikali utamaduni huo wa kunyonya matiti za wanawake baada ya kuzaa wakisema ni utamaduni wa tangu jadi na wazee wanahakikisha umepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
  • Wanawake wakanusha ripoti za madaktari kuwa utamaduni huo huathiri afya ya watoto wadogo wakisema wamezaa watoto waliogawana matiti na waume zao na wote wako buheri wa afya
  • Utamaduni huu hufanywa kisiri na wanakijiji wengi huogopa kuuzungumzia hadharani kwa hofu ya kuadhibiwa na wazee

MAAFISA wa afya eneo la Butere katika Kaunti ya Kakamega wametamaushwa na tamaduni ya wanaume wa sehemu hiyo kushindana na watoto wao wachanga kunyonya maziwa kutoka matiti ya wake zao wanapojifungua.

Wahudumu hao wanasema tabia hiyo, ambapo baba na mtoto kila mmoja hutengewa titi lake, imechangia kudhoofika kwa afya ya watoto wengi eneo hilo kutokana na kukosa kunyonya maziwa ya kutosha.

Lakini kulingana na wanaume waliohojiwa na Taifa Leo, haja yao si kunywa maziwa lakini wananyonya matiti za wake zao ili kuondolea mikosi mama na mtoto aliyezaliwa.

Pia, wanaume hao, ambao hawakutaka kutajwa majina kwa hofu ya kuvamiwa na wanakijiji kwa kufichua utamaduni huo, walisema hunyonya matiti za wake zao ili kuzuia kuyeyuka kwa ashiki za mapenzi za mama baada ya kuzaa.

Mmoja wa wanaume hao mwenye umri wa miaka 57 na baba ya watoto watano alitetea utamaduni huo wa kunyonya matiti za wanawake baada ya kuzaa akisema umekuwa tangu jadi na wazee wanahakikisha umepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Nilifuzwa utamaduni huu na babangu baada ya mke wangu kuzaa mtoto wa kwanza. Aliniambia kuwa kunyonya matiti ya mke wangu baada ya kuzaa ni muhimu kwa uzima wake na wa mtoto aliyezaliwa,”alieleza.

Aliongeza kuwa hatari iliyoko ni kuhakikisha mtoto hanyonyi titi linalonyonywa na baba. “Lazima mama awe makini sana kwa sababu mtoto akinyonya titi lililonyonywa na baba atakufa, na ni laana kwa hiyo familia,” alielezea mzee huyo.

Wataalamu wa kiafya wanasema kuwa hali hii inasababisha watoto kupata matatizo ya kiafya kwa kukosa kunyonya maziwa ya kutosha.

 

Kampeni ya kuzima utamaduni

Mnamo 2014, maafisa wa afya katika eneo la Butere wakiongozwa na Oliver Walutila walianzisha kampeni za kukomesha utamaduni huo wakisema unachangia ongezeko la vifo vya watoto wachanga.

“Uzima wa mtoto unategemea maziwa ya mama kwa hivyo akiachiwa tu titi moja huwa hapati lishe ya kutosha na virutibishi vinavyohitajika mwilini. Hali hii husababisha mtoto kukosa kinga ya kutosha anapokua,” Bw Walutila anasema.

Dkt Donald Musi anayesimamia kituo cha matibabu cha Yatta Plateau  anapuuzilia mbali utamaduni huo akisema ni kawaida wanaume kuvutiwa na matiti ya wanawake yanaponenepa baada ya kuzaa lakini hawafai kunyonya maziwa ya mtoto.

“Watoto wa kiume hupata mvuto kwa wanawake wakiwa wadogo, hali inayofahamika kama Oedipus Complex.  Hali hii husababishwa na mtoto kunyonya matiti pamoja na kuishika kila wakati akiwa mdogo, hali inayofanya apate ashiki za kimapenzi bila hata kujua,” anaelezea Dkt Musi.

Kwa mujibu wa Dkt Musi, inakubalika kiafya wanaume kuonyesha mapenzi kwa wake zao kwa kunyonya matiti zao lakini hawaruhusiwi kufanya hivyo baada ya mke kujifungua.

 

‘Hakuna athari mbaya’

Baadhi ya wanawake katika sehemu hiyo wanaunga mkono utamaduni huo. Bi Joyce Osiyo, mfanyabiashara mjini Butere anakanusha ripoti za madaktari kuwa utamaduni huo huathiri afya ya watoto wadogo akisema amezaa watoto wawili waliogawana matiti na mumewe na wote wako buheri wa afya.

“Kando na umuhimu wa kuzuia mikosi baada ya kujifungua, tamaduni ya kunyonywa matiti na mume wangu ilisaidia kudumisha ashiki za mapenzi baada ya kuzaa. Matiti ni kiungo muhimu cha mapenzi na utamaduni huu unasaidia kulinda ndoa kwa kudumisha mapenzi hata wakati mama amejifungua,” alisema Bi Osiyo.

Hata hivyo Mzee Waziri Mohammed mwenye umri wa miaka 82 anakemea utamaduni huo akisema ni kinyume na maadili ya jamii ya Waluhya.

“Utamaduni wa Waluhya hauruhusu mambo kama haya. Matiti ni kama sehemu za siri na mtoto hapaswi kutumia kiungo kinachotumiwa na babake, atakufa,” anasema Mzee Mohammed.

 

Kulaani watoto

Kauli ya Bw Mohammed inaungwa mkono na Musa Hamisi, 64, anayesema kuwa matiti ya mama hutumiwa mara nyingi kulaani mtoto anayevuka mipaka ya ushauri wa mamake.

“Mama akikerwa sana kwa kutoambilika kwa mwanawe, anatingisha matiti aliyoyanyonya mtoto huyo na kumlaani,” anasema Bw Hamisi.

Utamaduni huu hufanywa kisiri na wanakijiji wengi huogopa kuuzungumzia hadharani kwa hofu ya kuadhibiwa na wazee.

Ili kupunguza visa hivyo vya kina baba kunyonya maziwa ya watoto wao, mnamo 2014 serikali ya Kaunti ya Kakamega ilianzisha kampeni ya kuhamasisha kuhusu afya ya watoto wachanga kwa kuwapa akina mama wajawazito msaada wa pesa ili kuhakikisha mtoto amekua bila changamoto za kiafya.

“Mpango huu unalenga kuhakikisha wototo wananyonyeshwa kikamilifu kwa miezi sita baada ya kuzaliwa ili kupunguza vifo vya watoto wachanga,” alisema Patrick Ongaya, afisa wa kaunti anayesimamia mpango huo.