Waiguru amtaka rais azungumzie mrithi wake

Waiguru amtaka rais azungumzie mrithi wake

Na GEORGE MUNENE

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru anatarajia Rais Uhuru Kenyatta kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wakenya wakati wa sherehe za Sikukuu ya Mashujaa katika uwanja wa Wang’uru leo Jumatano.

Gavana huyo alisema suala la urithi wa urais ni muhimu zaidi na kiongozi wa taifa anafaa kulizungumzia katika sherehe hizo.

Akiongea Jumanne katika kijiji cha Kang’aru katika eneobunge la Ndia alipozindua usambazaji wa dawa za thamani ya Sh38 milioni kwa vituo vya afya, Bi Waiguru hata hivyo aliwataka Wakenya kuwa na subira na wasubiri hotuba ya Rais.

Gavana huyo pia alimtaka Rais Kenyatta kuzungumzia hali ya uchumi na kafyu ambayo inaendelea kutekelezwa.

Bi Waiguru alikariri kuwa kaunti ya Kirinyaga imejiandaa kwa sherehe hizo ambazo zitavutia wageni kutoka pembe zote za nchi na ng’ambo.

“Kama kaunti tumeweka rasilimali na nguvu zetu zote kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafaulu,” akasema.

Gavana Waiguru alisema dawa hizo zitasambazwa katika hospitali za zahanati mbalimbali ili kusaidia katika shughuli za dharura.

Vile vile, gavana huyo alisema kwua kufikia jana, jumla ya watu 100,000 katika kaunti hiyo walikuwa wamepokea chanjo ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Hii, alisema, itawawezesha kuwa salama wakati wa sherehe za leo, zinazoandaliwa katika kaunti ya Kirinyaga kwa mara ya kwanza tangu uhuru.

Bi Waiguru alisema maelfu ya wageni wengi watazuru kaunti hiyo na ni muhimu kwao kuchukua hatua na kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona.

“Ilitubidi kuimarisha shughuli ya kutoa chanjo kwa watu wengi tuwezavyo ili wapate kinga kabla ya siku ya sherehe,” akaeleza huku akikariri kuwa viongozi wa eneo hilo wameungana kumkaribisha Rais na wageni wengine.

You can share this post!

Sherehe zatuliza vita vya ubabe Kirinyaga

Washukiwa kusalia seli siku 10

T L