Makala

Tofauti za Gachagua na Ndindi ni za kisiasa au kibinafsi?

May 18th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro wameibuka kama washindani wawili wa kujitafutia ushawishi wa siasa za Mlima Kenya.

Swali linalosumbua wengi na kukanganya hata wanasiasa wa eneo hilo ni kuhusu ni nani hasa kati yao wawili anawafaa zaidi katika mkondo wa siasa za sasa na za baadaye.

Huku Nyoro akiwa na umri miaka 38 kwa sasa, Bw Gachagua ana yake 59.

“Siasa za hawa wawili zina shida na kuna uwezekano kwamba hata sio wao wanapigana…kuna uwezekano wa mkono mwingine kutoka nje, kwa sababu Nyoro alienda kwa debe la 2022 na akawania ubunge wa Kiharu huku naye Gachagua akimenyana kuwa Naibu wa rais,” asema mchambuzi wa siasa za eneo hilo Njoroge Ngugi.

Bw Ngugi anasema kwamba “wote wawili (Gachagua na Nyoro) wanaelewa majukumu ya afisi walizochaguliwa kuhudumia na mgongano walio nao kwa sasa sanasana unachochewa na uchokozi, dharau na ubinafsi”.

Aidha, Ngugi alisema kwamba kuna uwezekano kwamba Nyoro anafadhiliwa na wengine nje au ndani ya siasa za Mlima Kenya ili kumdunisha Gachagua kwa manufaa pana ambayo bado hayajabainika.

Mbunge wa Kangema, Bw Peter Kihungi alisema kwamba “mimi sielewi haya mambo kabisa kwa kuwa nimeongea na Bw Nyoro na akaniambia kwamba hana vita na Bw Gachagua na hakuna yeyote ambaye ametuma kumhujumu Naibu wa Rais mashinani”.

Hata hivyo, Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu ametangaza hadharani kwamba shida ya mrengo wa Bw Nyoro na Bw Gachagua hutokana na imani ya uongozi.

“Tuliochaguliwa sio watoto na tuna mawazo yetu thabiti. Sisi sio wa kuambiwa kama watoto, unafaa ushauriane nasi ili tutoe mawazo yetu nawe utoe yako, hatimaye tujadiliane tupate uwiano. Huyu Gachagua hutubeba kama taka na ni mwingi wa vitisho, kisasi na dharau,” akasema Bw Nyutu.

Hali ilivyo mashinani ya Mlima Kenya ni kwamba kaunti nyingi zimeyumba kisiasa huku walio kwa nyadhifa wakiangalia kwa makini ni wapi upepo utavuma, ukichochewa na eneo ambalo athari zitakuwa.

Hali hiyo imesemwa kuzua misukosuko ya kisiasa katika kaunti nyingi za Mlimani, Murang’a, Meru, Kiambu, Nairobi na Nakuru zikiwa tayari zimetumbukia kwa mizozo ya uongozi.

Lakini cha maana ambacho wenyeji wanajiuliza ni kuhusu upepo huo ukivuma na uangamize au utawaze yeyote kati ya Gachagua na Nyoro, ni nani mfaafu zaidi.

“Bw Gachagua amekuwa akifichua jinsi amesaidia wengi Mlima Kenya kupata kazi katika serikali ya Rais William Ruto. Amekuwa akisema anapambana na makateli wa sekta ya kilimo kwa manufaa ya mkulima na pia kwamba mambo bado, mengi yaja,” asema aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi.

Bw Ngugi anasema kwamba “siasa za manufaa ni kuangalia yale ambayo yanaimarisha maisha ya watu kiuchumi wala sio kisiasa”.

Bw Ngugi ametahadharisha wenyeji Mlima Kenya wajichunge sana wasiingie katika mtego wa kupiga domo la siasa huku wakiangalia miaka ya utawala huu ikisonga pasipo maendeleo.

“Mimi ninaamini sana utaratibu wa mambo. Kwa sasa Bw Gachagua amechaguliwa kuwa Naibu wa Rais. Bw Nyoro amechaguliwa kuwa mbunge wa Kiharu. Bw Nyutu amechaguliwa kuwa Seneta wa Murang’a, mimi nikiwa nje ya ushawishi. Kwa sasa tunafaa kuheshimiana na kila mtu ahudumie majukumu yake pasipo mgongano ili watu wetu wanufaike,” akasema Bw Ngugi.

Aliongeza kwamba “ni kweli kwamba Bw Gachagua ana shida zake za kimaongezi na ni mchache wa busara katika kupalilia uhusiano mwema na wengi lakini kwa sasa tunafaa kuelewa kwamba hatuna nafasi ya kumng’atua hadi 2027”.

Bw Ngugi anasema kwamba 2027 ndio mwaka mzuri wa kuleta mijadala hiyo “kwa sasa tukimsukuma Bw Gachagua atuletee manufaa yote ambayo yanawezekana kwa mujibu wa kura za Mlima Kenya ndani ya serikali hii, naye Nyoro asukume eneo bunge lake lipate haki ya rasilimali kwa kuwa lina idadi kubwa ya watu”.

Bw Nyoro ndiye mbunge wa makao makuu ya kaunti ambayo ni Mji wa Murang’a na ambao hauna viwanda vya kuajiri wenyeji na pia kusaidia kuinua uchumi wa biashara za eneo hilo.

“Ni mji tu unaosifika kuwa na hospitali kuu ya kaunti ambayo hata haina huduma za picha, mochari mbili za uwezo wa mahasla na biashara ambazo husaidiwa na wanafunzi walio katika taasisi za elimu hapa,” asema mwenyeji, Bowen Kiragu.

Mbunge wa Maragua, Bi Mary wa Maua alisema kwamba “tunachotaka ni mwanasiasa akisimama anatuonyesha yale amefanyia watu wetu ya kimaendeleo na tujichunge sana tusiingie katika mtego wa kupigana sisi kwa sisi ili tukose mwanya wa kudai maendeleo”.

Huku eneobunge la Mathira, atokako Bw Gachagua, likilizidi Kiharu kwa Nyoro kimaendeleo, tofauti zao wawili ni kama mbingu na ardhi.

“Kaunti ya Murang’a inakumbwa na umaskini kwa kuwa hakuna viwanda vya kuajiri wasio na ajira. Wizi wa mifugo na mavuno uko juu huku, na vilevile kero ya kusambaratika kwa bei ya bidhaa za kilimo likiwa donda sugu,” asema mwenyekiti wa baraza la Agikuyu Bw Wachira Kiago.

Bw Kiago alisema kwamba mwanasiasa yeyote anayelenga kujitetea kwa jamii, anapaswa kwanza atekeleze maendeleo kwake na kwa eneo ili wenyeji wafanye maamuzi yao kwa msingi wa manufaa.

“Hii ndiyo sababu hadi sasa wenyeji wanang’ang’ania mapenzi kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kuwa aliyoyafanya mashinani bado yanaonekana na hayajazidiwa umaarufu na utawala huu,” asema Bw Kiago.

Alisema kwamba “kwa sasa Bw Gachagua na Bw Nyoro wana nafasi nzuri kutekeleza mambo ya kimaendeleo eneo hilo na wakishirikiana wasaidie Mlima Kenya kuafikia makubwa ya kisiasa 2032”.

Alisema Bw Nyoro akiwa ndiye kinara wa bajeti naye Gachagua akiwa Naibu wa Rais, wana uwezo wa kumsukuma Rais Ruto kufanyia haki maeneo yote 11 ya Mlima Kenya kwa kuyapa viwanda, miradi na mapochocho mengine kimaendeleo.

“Hii vita inaonekana kuwa ya ubinafsi tu na haina manufaa kwetu kama jamii. Haifai kupewa nafasi ya kunawiri, lakini hivyo sio kusema nao wawe na kiburi, dharau na maongezi ya ovyo wasiwajibike na warekebike,” akasema.

Hofu kubwa ni kwamba migawanyiko hiyo ikipewa nafasi ya kukita mizizi eneo hilo basi litageuka kuwa mnara wa babeli na hatimaye katika chaguzi za 2027 na 2032, lijipate katika mahangaiko ya kutojielewa huku madalali wa kisiasa wakinufaika kivyao.

“Ushauri wangu kwa Bw Nyoro ni kwamba anajua vizuri hawezi kuwa rais mwaka wa 2027. Hali hii si tofauti na ya Bw Gachagua. Siasa za 2032 ziko mbali. Umoja wa Mlima Kenya ndio ngao yetu ya kukabiliana na 2027 na 2032. Kwa sasa, wote wawili hawajaafikia viwango vya kuongoza taifa hili na wanafaa kuzidisha bidii kujipa tajiriba,” asema aliyekuwa mkuu wa eneo la Nairobi kiutawala Bw Joseph Kaguthi.