Tofauti zaibuka kuhusu uteuzi Kadhi wa kike

Tofauti zaibuka kuhusu uteuzi Kadhi wa kike

KALUME KAZUNGU na FARHIYA HUSSEIN

PENDEKEZO la kuruhusu wanawake wateuliwe kwa nafasi ya Kadhi Mkuu au Kadhi, linazidi kuibua mitazamo tofauti miongoni mwa Waislamu.

Baadhi ya viongozi wa Kiislamu, wasomi na wahubiri wamepinga pendekezo hilo ambalo lilikuwa limeungwa mkono na Kadhi Mkuu, Sheikh Ahmed Muhdhar.

Wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Aden Duale, wamedai kuwa hatua hiyo ni kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.

“Hilo halipatikani katika Quran wala mafundisho ya Mtume. Kama Martha Koome alichaguliwa kuwa Jaji Mkuu haimaanishi inafaa pia tuwe na Kadhi wanawake. Mahakama ya Juu haihusu mambo ya kidini jinsi ilivyo katika Mahakama za Kadhi,” akasema Bw Duale.

Alieleza kuwa sababu zake kupinga pendekezo hilo ni kuwa hakuna wanawake Waislamu ambao hukubaliwa kuongoza shughuli kama vile kufunganisha watu ndoa, talaka au urithi ambazo hushughulikiwa sana katika mahakama hizo.

Watetezi wa pendekezo hilo wakiongozwa na wasomi wa kike Waislamu walikuwa wamesema Mahakama ya Kadhi ni sawa na ya Hakimu kwa hivyo ikiwa kuna mwanamke aliyehitimu kwa Sharia za Kiislamu, anastahili kupewa nafasi.

Katika Kaunti ya Lamu, wahubiri wa Kiislamu waliomba wasomi wanawake nchini waache kushinikiza kuajiriwa kuwa Kadhi Mkuu wala Kadhi.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wahubiri Pwani, tawi la Lamu, Bw Mohamed Abdulkadir, viongozi hao walisema mahakama hiyo haifai kuchukuliwa kama nyingine za ‘kidunia’.

Alisisitiza kuwa dini ya Kiislamu inawatambua na kuwaheshimu wanawake katika majukumu yao, na jukumu la Kadhi si mojawapo.

“Nashauri watu wajihadhari sana wanapojadili masuala ya dini hya Kiislamu. Inafaa watofautishe Mahakama ya Kadhi na zile za kawaida. Mahakama ya Kadhi ni ya masuala ya kidini. Hakuna vile tunaweza kukubali kuwa na Kadhi wanawake. Quran Takatifu na hata mafundisho ya Mtume wetu yako wazi kuhusu suala hilo,” akasema Bw Abdulkadir.

Alikosoa wanaotoa mfano wa mataifa kama vile Misri, Malaysia, Sudan, Jordan, Tunisia, Uturuki, Palestina na mengine ambayo yana Kadhi wanawake akisema mataifa hayo yana sababu zao.

“Masuala ya kidini si kama vile ya BBI au uchaguzi. Katika historia ya Kiislamu hakujawahi kuwa na Kadhi mwanamke kwa hivyo hilo halifai kufanyika sasa,” akaongeza.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), tawi la Lamu Magharibi, Noordin Saney, alidai kuwa wanawake wenye azma ya kupigania nyadhifa hizo wamepotoka hasa kimaadili ya dini.

Kwa upande wake, msomi wa dini ya kiislamu kisiwani Lamu, BwMahmoud Ahmed Mau, alisema suala la iwapo mwanamke afaa au kutofaa kushikilia wadhifa wa kadhi au kadhi mkuu bado liko kwenye mizani kwani hata wasomi wenyewe wa dini ulimwenguni kote bado hawajafikia makubaliano.

Sheikh Mau alisema Quran pia haijaweka bayana iwapo mwanamke afaa au hafai kushikilia wadhifa wa kadhi au kadhi mkuu.

Mtetezi wa Haki za Kibinadamu na mpigania jinsia ya kike, Raya Famau pia aliunga mkono msimamo wa viongozi hao wa kidini wa Lamu kwamba wadhifa wa kadhi uachiwe wanaume.

Bi Famau alisema yuko tayari kupigania haki na usawa wa kijinsia kwa sekta zote lakini akasisitiza kuwa kwa upande wa makadhi lazima wanawake waheshimu na kuyaacha majukumu hayo kutekelezwa na wanaume.

You can share this post!

Tanzania mbioni kuunda chanjo yake ya corona

Mizozo ya wanasiasa yaua ziara ya Uhuru Ukambani