Michezo

Tokyo Marathon 2021 yaahirishwa ifanyike baada ya Olimpiki za Tokyo, Japan

October 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MAKALA yajayo ya mbio za Tokyo Marathon yameahirishwa hadi Michezo ya Olimpiki ya Tokyo iliyoratibiwa upya kwa sababu ya corona inogeshwe kwanza hapo mwakani.

Haya ni kwa mujibu wa waandalizi ambao wameshikilia kwamba ujio wa janga la corona utaendelea kuathiri kalenda za michezo mbalimbali kwa kipindi cha misimu kadhaa ijayo.

Awali, mashindano ya Tokyo Marathon yalikuwa yafanyike Machi 7, 2021 na yalitarajiwa kuleta pamoja zaidi ya wanariadha 38,000 wakiwemo wengi wa haiba kubwa zaidi kutoka kote duniani.

Hata hivyo, uchache wa watu wanaokubaliwa kuingia nchini Japan na ukali wa kanuni zilizowekwa ili kudhibiti maambukizi zaidi ya corona sasa umechangia michezo hiyo kupangiwa upya hadi Oktoba 17, 2021.

Haya ni kwa mujibu wa waandalizi na wadhamini wa mbio hizo, Tokyo Marathon Foundation.

Nyingi za marathon kuu duniani, isipokuwa ya London iliyojumuisha wanariadha wa haiba kubwa zaidi pekee mnamo Oktoba 4, ziliahirishwa au kufutuliwa mbali kabisa kwa sababu ya corona.

Makala ya Tokyo Marathon mwaka huu wa 2020 yalifanyika Machi na yanogeshwa na wanariadha wachache zaidi wa haiba kubwa katika historia – 200.

Kwa mujibu wa waandalizi, hatua ya kuruhusu mashindano ya mwaka ujao kufanyika baada ya Olimpiki itawapa wanariadha jukwaa zuri zaidi la kushiriki mbio hizo kwa wingi ila idadi ya watakaoshiriki bado haijaamuliwa.

Olimpiki za Tokyo, Japan zilizoahirishwa mwaka huu sasa zitaandaliwa mnamo Julai 23, 2021. Hata hivyo, tarehe hiyo huenda ikabadilishwa tena kutegemea viwango vya maambukizi na hali itakayokuwa imezuliwa na corona kote duniani kufikia wakati huo.