MakalaSiasa

TOM MBOYA: Mtetezi wa haki za wafanyakazi nchini na kimataifa

April 14th, 2019 4 min read

Na KENYA YEARBOOK

Thomas Joseph Mboya atakumbukwa kama mmoja wa mawaziri machachari na wajasiri ambao Kenya imewahi kupata. Wakati wa uchaguzi mwaka wa 1963 aliteuliwa waziri wa Haki na Masuala ya Katiba. Mnamo 1965, alihamishiwa Wizara ya Mipango ya Kiuchumi.

TJ, alivyojulikana na wengi, alizaliwa Agosti 15 1930 akiwa mvulana kifungua mimba wa Leonard Ndiege na Marcela Awuor ambao walitoka kisiwa cha Rusinga mkoani Nyanza.

Wazazi wake walithamini elimu na ingawa walikuwa vibarua katika shamba la mikonge eneo la Kilimambogo, karibu na Thika, walihakikisha alipata elimu katika shule za mishenari za kanisa Katoliki.

Mboya alianza masomo akiwa na umri wa miaka tisa. Baba yake alimpeleka shule ya mishenari Machakos iliyosimamiwa na kasisi kutoka Ireland ambapo alisomea kwa miaka mitatu.

Mnamo 1942, alihamishiwa shule ya misheni ya St Mary, Yala, Nyanza. Ni akiwa St Mary ambapo alianza kusoma Kiingereza na Historia. Kauli mbiu, “Hakuna kutozwa kodi bila kuwakilishwa,” ya ukoloni kutoka Amerika, ilijikita katika akili yake akiwa na umri mdogo.

Alifanya vyema kwenye mtihani wa Kenya African Primary Examination mwaka wa 1945 na akajiunga na Holy Ghost College (Mangu), shule ya kanisa Katoliki iliyokuwa ikifanya vyema Mkoa wa Kati mwaka wa 1946.

Mboya alikuwa mmoja wa waigizaji mashuhuri na washiriki mijadala katika shule hiyo akiigiza Mark Twain.

Alivutiwa mno na yaliyoendelea Ulaya na alipendezwa na mfalme wa Ufaransa Napoleon Bonaparte, Rais wa Amerika Abraham Lincoln na mwanaharakati wa haki za watu weusi Booker T. Washington.

Mboya alisema na kukariri hotuba za Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill alizotoa wakati wa vita miongoni mwa nyingine.

Hata hivyo, mapato yake haba yaliisha mwaka wake wa mwisho na hakuweza kufanya mtihani wa kitaifa ambao ungemwezesha kujiunga na chuo kikuu. Hii haikuzima ari yake ya kufaulu katika maisha yake.

Mnamo 1948, alijiunga na chuo cha Royal Sanitary Institute Medical Training School for sanitary inspectors na kufuzu kama mkaguzi mnamo 1950.

Baadaye alifanya kazi katika Baraza la Jiji la Nairobi kwa miaka miwili na nusu. Alijiuzulu na kuwa katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa serikali ambacho alikuwa ameunda.

Baadaye alijiunga na National African Local Government Servants Association na ndani ya mwaka mmoja alichaguliwa makamu- rais.

Mnamo Novemba 1953, alichaguliwa katibu mkuu wa Kenya Federation of Labour na kuhudumu hadi 1962 alipojiuzulu kujiunga na baraza la mawaziri kama waziri wa leba katika serikali ya muungano.

Katika miaka ya 1950s, Mboya alikuwa ameamua kuwa maisha yake ya uanaharakati yangeanza katika chama cha wafanyakazi.

Mnamo 1952, nyota yake iling’aa alipounda chama cha Kenya Local Government Workers Union, wakati ambao serikali ya kikoloni ilikuwa imetangaza vita dhidi ya Mau Mau na kukamata na kuzuilia wapiganiaji uhuru wa kitaifa na wafuasi kama vile Kenyatta na Achieng’ Oneko.

Mboya alijijengea jina nchini na kimataifa miaka ya hamsini na sitini, kwa kutumia cheo chake katika vyama vya wafanyakazi wakati wa hali ya hatari, mojawapo ya enzi za giza katika historia ya Kenya.

Baadaye aliteuliwa mwakilishi wa Kenya katika shirikisho la kimataifa la vyama huru vya wafanyakazi, wadhifa ambao alitumia kuimarisha kazi yake.

Uamuzi wa kwanza wa kisiasa wa Mboya ulichochewa na kutangazwa kwa hali ya hatari. Kwa sababu hiyo inasemekana alienda katika ofisi za chama cha Kenyatta’s Kenya African Union (KAU) jijini Nairobi na kujiunga na chama hicho ambacho wanachama wake walikuwa wamekamatwa na kutupwa kizuizini.

Mboya alikubali wadhifa wa mweka hazina wa KAU na akaanza kuongoza upinzani dhidi ya utawala wa Mwingereza.

Akiungwa mkono na washirika wake wa kimataifa na hasa chama cha British Labour Party, Mboya aliunganisha vyama vitano vikuu chini ya mwavuli wa Kenya Federation of Labour (KFL), wakati huo KAU kilipopigwa marafuku mwaka huo na kuacha KFL kikiwa chama kikumbwa cha waafrika kilichotambuliwa nchini.

Kuanzia wakati huo alikuwa mwanasiasa maarufu, kutokana na ujasiri wake katika vyama vya wafanyakazi, kupinga kutimuliwa kwa halaiki, kuzuiliwa katika kambi na kushtakiwa kisiri.

Mnamo 1955, chama cha British Labour Party kilimteua kwenda kusoma kwa mwaka mmoja katika chuo cha Ruskin College cha chuo kikuu cha Oxford ambapo alisomea masuala ya usimamizi wa wafanyakazi. Ufadhili huo ulitoka kwa muungano wa vyama vya wafanyakazi vya Uingereza.

Aliporudi Kenya 1956, Mboya alipata kuwa Mau Mau ilikuwa imezimwa na maelfu ya wanachama wake kuuawa na wengine wengi kusukumwa kuzuizini. Hii ilimfanya yeye na wengine kuunda chama cha People’s Convention Party (PCP) mnamo 1957 ambacho kilikuwa cha Nairobi pekee.

Baadaye alitumia chama hicho kuchaguliwa mwanachama wa Legco akiwa mmoja wa waafrika wanane. Akiwa Legco, alitetea waafrika kupata haki sawa na wengine.

Juhudi zao zilizaa matunda. Idadi ya wawakilishi waafrika iliongezeka kutoka nane hadi 14 sawa na wazungu ingawa walikuwa wakiwakilisha zaidi ya Waafrika milioni sita dhidi ya wazungu 6,000.

Wakati huo alibobea na akaanza uhusiano na viongozi wa mataifa mengine Afrika kama Kwame Nkrumah wa Gold Coast ( baadaye Ghana). Mnamo 1958, wakati wa kongamano la All African Peoples’ Conference lililoitishwa na Nkrumah jijini Accra, aliteuliwa mwenyekiti akiwa na miaka 28.

Baadaye alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “Hiyo ilikuwa siku ya kujivunia katika maisha yangu!”

Waliomfahamu wanasema kwamba alikuwa mtulivu na alikuwa akijiamini. Alikuwa akiendesha kampeni zake kwa uchangamfu, ambao ulimwezesha kushinda kiti cha Nairobi Central (Kamukunji).

Pia alionekana mara kwa mara katika runinga ya Uingereza. Mnamo 1959, alienda kwa ziara ya kutoa mihadhara Amerika ambapo alitunukiwa digrii ya heshima ya uzamili kuhusu masuala ya sheria kutoka chuo kikuu cha Howard, Washington DC.

Mboya alianza mmoja wa miradi ya masomo kuwahi kufanyika Afrika Mashariki na Kati.

Aliongoza wakfu wa kuwapa wanafunzi wa Afrika kusomea Amerika ambao ulichanga pesa kusaidia wanafunzi kutoka Afrika kusomea vyuo vikuu vya Amerika. Mnamo 1959, Wakenya 81 walienda kusomea vyuo vikuu vya Amerika.

Obama Snr, baba ya Rais wa Amerika Barrack Obama ambaye alikuwa rafiki ya Mboya, alikuwa ameenda Amerika mwaka mmoja uliotangulia chini ya ufadhili uliotolewa na Wamishenari.

Mnamo 1960, Mboya alimtembelea Seneta John F. Kennedy kutafuta msaada na wakfu wa Kennedy Foundation na ukakubali kusaidia awamu ya pili ya wanafunzi Waafrika kusomea Amerika.

Mradi huo ulipanuliwa hadi Uganda, Tanganyika na Zanzibar (sasa Tanzania), Rhodesia Kaskazini (Zambia), Rhodesia Kusini (Zimbabwe) na Nyasaland (Malawi). Wanafunzi Waafrika 230 walinufaika 1960 na mamia ya wengine kati ya 1961 na 1963.

Lakini juhudi za Mboya hazikuwa Amerika pekee. Mnamo Januari 1961, alienda Mashariki hadi India na kukutana na Waziri Mkuu Jawaharlal Nehru, na kutangaza kuwa Kanu ilipanga kupeleka wanafunzi kutoka Afrika kusomea masuala ua maendeleo.

Mboya alipokelewa vyema katika hafla iliyoandaliwa na Indian Council for Africa, na alipata zawadi moja ya kisiasa- Pandit Nehru alihimiza serikali ya kikoloni kumwachilia Kenyatta kutoka kizuizini.

Mboya alikuwa mmoja wa wanachama wa Legco ambao walikuwa wakipigana ili Kenyatta aachiliwe wakitumia kauli mbiu ya “Uhuru na Kenyatta.” Juhudi zao zilizaa matunda Agosti 21, 1961, wakati Kenyatta na wenzake walipoachiliwa. Kuanzia wakati huo, Kenyatta alichukua hatamu na kuelekeza nchini changa hadi ikapata uhuru.

Wakati huo, wimbi la mabadiliko lilikuwa likivuma kote Afrika na Kenya haikuachwa nyuma. Mnamo 1960, chama cha Mboya (PCP) kiliungana na KAU na Kenya Independent Movement kuunda Kenya African National Union (Kanu) ili kujiandaa kwa kongamano la Lancaster House kuhusu katiba na uhuru.

Mboya alichaguliwa katibu mkuu. Kwenye uchaguzi wa 1961, Mboya alishinda kiti cha eneobunge la Nairobi Central akiwa na kura 3,100 dhidi ya 2,668 za Munyua Waiyaki na 1,577 za Martin Shikuu wa chama cha Kenya African Democratic Union.

Mnamo Januari, 1962, alimuoa Pamela Arwa Odede. Waliohudhuria harusi walikuwa wanasiasa watajika nchini Kenyatta, Gichuru, Odinga, Kabaka wa Uganda, na Dereck Erksine na Bruce McKenzie, wazungu wawili ambao walikuwa wanachama wa Kanu katika Legco.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke