Michezo

Tomas Soucek kuchezea West Ham msimu ujao

July 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WEST Ham United wamemsajili rasmi kiungo matata mzawa wa Jamhuri ya Czech, Tomas Soucek, 25, aliyekuwa akiwachezea kwa mkopo kutoka Slavia Prague kwa mkataba wa miaka minne.

Uhamisho wa nyota huyo aliyejiunga na West Ham mnamo Januari 2020 umerasimishwa kwa kima cha Sh2.7 bilioni.

Soucek anajivunia kuwafunga wapinzani wa West Ham mara tatu tangu kurejelewa kwa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 17, 2020.

Ukubwa wa mchango wake chini ya kocha David Moyes uliwawezesha West Ham kuponea chupuchupu kushushwa ngazi kwenye kampeni za EPL msimu huu. Sare ya 1-1 waliosajili dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford mnamo Julai 22, 2020 iliwapa uhakika wa kusalia katika EPL kwa msimu wa tisa mfululizo huku wakisalia na mechi moja zaidi msimu huu.

“Ushawishi wa Soucek uwanjani umekuwa mkubwa. Alichangia sana ushindi wa hivi karibuni tuliosajili dhidi ya Chelsea, Newcastle na Watford. Nilipokubali kudhibiti mikoba ya West Ham, nilisadikisha usimamizi kuhusu haja ya kusajiliwa kwa kiungo ambaye angeibua ubora zaidi wa Declan Rice na Mark Noble.

Ni afueni tele kwamba sogora aliyefanya kazi hiyo kwa mafanikio zaidi ni Soucek ambaye kwa sasa amekubali mkataba wa kudumu,” akasema Moyes ambaye pia amewahi kuwatia makali vijana wa Everton, Real Sociedad, Sunderland na Manchester United.