Tope la Jubilee latesa Raila

Tope la Jubilee latesa Raila

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

DHAMBI zilizotendwa na serikali ya Jubilee zinatishia umaarufu wa kiongozi wa ODM Raila Odinga huku akijiandaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Tangu ilipochukua uongozi wa nchi 2013, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto imekuwa ukihusishwa na maovu mengi yanayowaandama Wakenya hadi sasa.

Hili ni kinyume na ahadi nyingi walizotoa kwa wananchi kuhusu namna ambapo wangeyaboresha maisha yao.

Baadhi ya ‘dhambi’ zinazohusishwa na utawala huo ni kupanda kwa gharama ya maisha, kuongezeka kwa deni la nchi, ongezeko la sakata za ufisadi, jaribio la kuibadilisha Katiba, kubomoa makazi ya wananchi na matumizi ya polisi kuwahangaisha raia.

Serikali ya Jubilee ilipochukua hatamu za uongozi 2013, deni la kitaifa lilikuwa Sh1.7 trilioni na sasa limefikia Sh7.12 trilioni na kuwatwika Wakenya mzigo mzito wa madeni.

Mnamo Januari 2021, Rais Kenyatta alipokuwa akihojiwa na vituo vya habari vinavyotumia lugha ya Kikuyu, alikiri kwamba Sh2 bilioni za walipa ushuru zinaibwa kila siku na wafisadi serikalini. Kauli hiyo imefasiriwa kuwa ameshindwa kukabiliana na ufisadi nchini.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hatari inayomwandama Bw Odinga ni kimya chake kuhusu baadhi ya maovu hayo, ikizingatiwa kwamba alikuwa akiukosoa utawala huo kabla ya handisheki mnamo 2018.

Rais Kenyatta mara kadhaa amenukuliwa akisema kuwa Bw Odinga yuko serikalini licha ya kiongozi huyo wa ODM kushikilia kwamba angali kwenye upinzani.

Wabunge David Sankok (Maalum) na Rashid Kassim Amin walidai kwamba kiongozi wa ODM Raila Odinga ndiye wa kulaumiwa kwa maovu yanayotendeka katika serikali ya Jubilee.

“Hili tatizo la ongezeko la bei ya mafuta lilitokana na handisheki. Sasa Wakenya hawafai kumpa Raila urais 2022 kwa sababu alitelekeza wajibu wake kwa kuingia serikalini 2018,” akasema Bw Sankok, mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto, alipokuwa akichangia Bungeni Jumanne.

Kwa upande wake Bw Kassim alimtaka Bw Odinga astaafu pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kwa sababu alisaliti Wakenya alipoingia serikalini.

“Kando na bei ya mafuta sakata za ufisadi kama ile iliyotokea katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa nchini (KEMSA) ingedhibitiwa ikiwa Raila hangeingia serikalini. Kwa hivyo, haina haja kwake kutaka urais tena; aende nyumbani pamoja na Uhuru,” Mbunge huyo wa chama cha Wiper akasema huku akionekana mwenye hamaki.

Wadadidisi wanasema kuwa tope la Jubilee limesababisha umaarufu wa Bw Odinga kupungua nchini.

“Katika muhula wa kwanza wa serikali ya Jubilee, Raila alikuwa akijitokeza wazi kuikosoa na kuikashifu serikali kutokana na maovu yaliyokuwepo kama ufisadi na kucheleweshwa kwa miradi muhimu ya maendeleo. Hata hivyo, Raila na chama cha ODM wamejivika upofu dhidi ya maovu yote yanayohusishwa na serikali hiyo,” akasema mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ Ijumaa.

Akaongeza: “Hili linamaanisha kuwa katika muhula wa pili wa utawala wake, Jubilee imefanya maovu mengi bila kukosolewa kutokana na kimya cha Bw Odinga na hatua yake kutotumia ushawishi wa kisiasa alio nao kuikosoa.”

Jubilee imekuwa ikilaumiwa kwa kupanda kwa gharama ya maisha, baada ya wabunge kupitisha Miswada wa Fedha 2018, ambao uliipa serikali nafasi ya kuongeza ushuru kwa bidhaa muhimu.

Wakati wa kikao cha kujadili mswada huo katika Bunge la Kitaifa, wabunge wa ODM waliupitisha mswada huo bila kujali madhara ambayo ungewaletea Wakenya.

Bw Odinga pia analaumiwa kwa kunyamazia baadhi ya sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikiendelea katika serikali hiyo kama uporaji wa fedha za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

“Katika muhula wa kwanza, Bw Odinga ndiye aliyefichua sakata ya ufisadi kuhusu mkopo tata wa Eurobond. Hali ni kinyume sasa kwani sauti yake huwa haisikiki tena. Taswira na sifa yake kama mtetezi wa wananchi inaendelea kupungua,” asema Bi Mutheu Matheka, aliye mchanganuzi wa siasa na mtaalamu wa masuala ya utawala.

Wadadisi wanaeleza “dhambi kuu” ambayo inamhusisha Bw Odinga na makosa ya Jubilee ni kukubali kuwa miongoni mwa wale walioshinikiza mageuzi ya Katiba kupitia Mchakato wa Kuibadilisha Katiba (BBI).

“Ingawa awali mchakato huo ulionekana kama njia ya kuleta umoja na maridhiano, hilo lilibadilika kabisa wakati Dkt Ruto na waandani wake walidai kutengwa kutoka serikalini. Msimamo wao (Uhuru na Raila) kuhusu BBI ulibainika kutokuwa wa kweli ulipoharamishwa na mahakama,” asema Bi Mutheu.

Wadadisi wanasema tatizo kuu linalomwandama Bw Odinga ni jinsi atakavyojitenga na maovu hayo, ikizingatiwa amekuwa mtetezi mkubwa wa serikali ya Jubilee na kuonekana kama sehemu yake.

Hata hivyo, mdadisi wa siasa Macharia Munene anasema kuwa kinyume na dhana hizo, Raila “hajajipaka tope kisiasa.”

“Badala ya kupoteza, Raila amejijenga sana kisiasa kutokana na ushirika wake na Rais Kenyatta. Ikiwa atashindwa kisiasa kwenye uchaguzi ujao, hilo halitatokana na ushirikiano wake na Jubilee, bali litachangiwa na sababu nyingine, kwa mfano jinsi atakavyoendesha kampeni zake,” akasema Prof Munene kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Anamtaja Raila kuwa mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa katika siasa, mwenye uwezo wa kutumia ushawishi wake kujizolea umaarufu katika sehemu zote nchini.

You can share this post!

KAMAU: Ni aibu kuwatelekeza mashujaa waliopigania uhuru

Brazil yaita kambini masogora wanane wanaopiga soka...