Michezo

Torreira atajwa injini ya kuimarika kwa Arsenal

December 11th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa Arsenal Lucas Torreira ndiye mchezaji bora wa mwezi Novemba katika kikosi cha Arsenal.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 22 amekuwa katika kiwango cha kutisha kwenye safu ya kati ya The Gunners,  uchezaji huo bora ukimvunia tuzo hiyo ya hadhi katika kikosi cha mibabe hao wanaopania kushinda ligi ya EPL kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2003.

Mnamo Novemba 3, 2018 Torreira,  alitajwa  mchezaji bora wa mechi kwenye sare ya kuridhisha yas 1-1 dhidi ya Liverpool. Alitajwa tena kama mchezaji bora wa mechi Arsenal ilipoadhibu Bournemouth 2-1 ugeni Novemba 29, 2018.

Raia huyo wa Uruguay aliwapiku mnyakaji Bernado Leno na kinda mwengine Rob Holding waliomaliza katika nafasi ya pili na tatu mtawalia baada ya mashabiki wa klabu hiyo kumpigia kura kwa wingi.