Michezo

Torreira mwili wa chuma katika ngome ya Arsenal

January 7th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

LUCAS Sebastian Torreira Di Pascua, 22, ni kiungo mzawa wa Uruguay ambaye kwa sasa anavalia jezi za Arsenal nchini Uingereza.

Akiwa miongoni mwa wachezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha Unai Emery mwanzoni mwa msimu huu, Torreira tayari amejipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Arsenal huku baadhi ya wadadisi wakiulinganisha uwezo wake na wa Patrick Vieira na Gilberto Silva.

Kwa mujibu wa Emery, uwezo wa Torreira wa kuwakabili vilivyo wapinzani, nguvu zake zisizokwisha kirahisi chini ya dakika 90 za mchezo na umahiri wake katika kutoa pasi za hakika ni sifa zitakazomfanya kuwa mchezaji wa kuwaniwa na vikosi maarufu za bara Ulaya kwa zaidi ya Sh9 bilioni mwishoni mwa msimu huu.

Torreira alianza kupiga soka ya kulipwa akivalia jezi za kikosi cha I.A. 18 de Julio of Fray Bentos nchini Uruguay kabla ya kujiunga na Montevideo Wanderes mnamo 2013. Miezi michache baadaye, alitua kambini mwa Pescara nchini Italia.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa msimu wa 2014-15 kupulizwa, alijiumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Pescara kabla ya kuwa kwenye benchi mnamo Oktoba 25, 2014.

Mchuano wake wa kwanza kambini mwa Pescara ni mechi ya Ligi ya Daraja ya Kwanza (Serie B) dhidi ya Varese mnamo Mei 16, 2015. Katika mechi hiyo, Torreira aliwajibishwa kwa jumla ya dakika 58 kabla ya nafasi yake kutwaliwa na Matteo Politano.

Mnamo Julai 1, 2015, aliingia katika sajili rasmi ya Sampdoria waliojinasia huduma zake kwa kima cha Sh600 milioni. Ingawa hivyo, alisalia kambini mwa Pescara kwa mkopo wa mwaka mmoja zaidi ili kujipa tajriba zaidi.

Mnamo Agosti 9, 2015, Torreira alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Sudtirol katika mchuano wa kuwania taji la Coppa Italia.

Baada ya kukamilika kwa kipindi chake cha mkopo kambini mwa Pescara, Torreira alirejea Sampdoria mnamo Julai 1, 2016. Mwezi mmoja baadaye, aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) dhidi ya Empoli uwanjani Carlo Castellani.

Baada ya kuridhisha vinara wa Sampdoria katika mchuano huo, alijipa uhakika wa kuunga na kukamilisha kikosi cha kwanza.

Ubunifu wake ulitegemewa pakubwa kambini mwa Sampdoria katika kampeni za msimu wa 2016-17. Mbali na kuchangia mabao, alipachika wavuni mabao muhimu katika mechi kadhaa, ikiwemo ile iliyomalizika kwa Sampdoria kusajili ushindi wa 3-2 dhidi ya Juventus mnamo Novemba.

Mnamo Julai 10, 2018, Torreira alisajiliwa na Arsenal kmwa kima cha Sh3.5 bilioni. Alikabidhiwa jezi nambari 11 ambayo hadi kutua kwake ugani Emirates, ilikuwa ikivaliwa na kiungo Mesut Ozil. Ozil badala yake alipokezwa jezi nambari 10 iliyokuwa ya kiungo Jack Wilshere aliyejiunga na West Ham United ya mkufunzi Manuel Pellegrini.

Torreira aliwajibishwa na Arsenal kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 12. Alitokea benchi kunako dakika ya 70 katika mchuano uliowashuhudia waajiri wake wakipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa mabingwa watetezi wa EPL, Manchester City.

Alichangia bao lake la kwanza la msimu katika mechi ya EPL iliyowakutanisha na limbukeni Cardiff City baada ya kumwandalia Alexandre Lacazette krosi safi katika ushindi wa 3-2 waliousajili ugani Emirates.

Mchuano wa kwanza uliomshuhudia akipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal ni kivumbi cha Ligi ya Uropa kilichowakutanisha na FC Vorskla Poltava. Katika mchuano huo uliowashuhudia Arsenal wakiwapepeta wapinzani wao 4-2, Torreira aliondolewa ugani kunako dakika ya 57 na nafasi yake kujazwa na kiungo Matteo Guendouzi.

Matokeo ya Torreira katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Arsenal dhidi ya Liverpool katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu ulimvunia sifa tele kutoka kwa mashabiki na wadadisi wa soka. Mnamo Desemba 2, alifunga bao lake la kwanza ndani ya jezi za Arsenal.

katika mchuano wa EPL uliowakutanisha na watani wao wa tangu jadi, Tottenham Hotspur uwanjani Emirates.

Katika mechi hiyo, Torreira alidhihirisha ustadi wake kwa kukamilisha krosi aliyomegewa na Pierre-Emerick Aubameyang na hivyo kumwacha hoi kipa Hugo Lloris katika ushindi wa 4-2 uliovunw ana Arsenal dhidi ya vijana hao wa kocha Mauricio Pochettino.

Mnamo Desemba 8, alifunga bao lake la pili dhidi ya Huddersfield katika kivumbi cha EPL kilichomshuhudia akitawazwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Japo alizaliwa Uruguay, Torreira ana usuli wake jijini Galicia, Uhispania alikozaliwa babu yake. Licha ya kuwa na uraia wa Uhispania, yalikuwa matamanio makubwa ya vinara wa soka nchini Italia kumshuhudia akivalia jeza za Azzuri.

Alipangwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Uruguay mnamo Machi 2018 katika mchuano wa kuwania taji la China Cup. Alitegemewa sana katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Uruguay dhidi ya Jamhuri ya Czech katika nusu-fainali za kipute hicho.

Mnamo Mei 2018, alijumuishwa katika kikosi cha wachezaji 26 waliounga timu iliyopeperusha bendera ya Uruguay katika fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.