Tottenham na Frankfurt waumiza nyasi bure katika pambano la UEFA nchini Ujerumani

Tottenham na Frankfurt waumiza nyasi bure katika pambano la UEFA nchini Ujerumani

Na MASHIRIKA

KOCHA Antonio Conte ametaka masogora wake wa Tottenham Hotspur kuwa wabunifu zaidi katika safu ya mbele baada ya kuwashuhudia wakipoteza nafasi nyingi za wazi katika mchuano wa Kundi D kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uliokamilika kwa sare tasa dhidi ya Eintracht Frankfurt mnamo Jumanne usiku nchini Ujerumani.

Matokeo hayo yaliacha Spurs katika nafasi ya pili kwa alama nne sawa na Frankfurt. Ni pengo la pointi mbili ndilo linatamalaki kati ya Spurs na viongozi wa Kundi D, Sporting Lisbon ya Ureno iliyotandikwa na Olympique Marseille 4-1 nchini Ufaransa.

Harry Kane, Son Heung-min na Ivan Perisic walizidiwa maarifa na kipa wa Frankfurt aliyepangua na kudhibiti mengi yao makombora yao mazito.

Chini ya kocha Antonio Conte, Spurs walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Arsenal kuwakung’uta 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 1, 2022. Frankfurt kwa upande wao walitarajia kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakipiga breki kasi ya Union Berlin wanaongoza jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa ushindi wa 2-0 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Pambano dhidi ya Spurs liliwapa Frankfurt jukwaa mwafaka la kushinda mechi yao ya nne mfululizo tangu wacharaze Olympique Marseille 1-0 katika UEFA mnamo Septemba 13 nchini Ufaransa. Kikosi hicho kilifungua kampeni za Kundi D katika UEFA kwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Sporting.

Spurs waliweka rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza cha Uingereza kupoteza dhidi ya Sporting katika UEFA baada ya kufinywa 2-0 mnamo Septemba 13. Kupigwa kwao na Arsenal kuliwasaza katika nafasi ya tatu ligini kwa alama 17, tatu nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Napoli yatoka nyuma na kudhalilisha Ajax mbele ya mashabiki...

Inter Milan yadidimiza matumaini ya Barcelona kutinga hatua...

T L