Tottenham wakomoa Watford na kudhibiti kilele cha jedwali la EPL

Tottenham wakomoa Watford na kudhibiti kilele cha jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

FOWADI Son Heung-min alifungia Tottenham Hotspur bao la pekee na la ushindi dhidi ya Watford katika mchuano wake wa 200 ndani ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumampili.

Ushindi huo uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa Spurs ya kocha Nuno Espirito katika mechi tatu za ufunguzi wa EPL msimu huu.

Vikosi vya EPL vinapoanza likizo fupi ili kupisha mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Spurs wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama tisa huku Watford wakikamata nafasi ya 12.

Nuno kwa sasa ndiye kocha wa pili wa Spurs baada ya Arthur Rowe mnamo 1949 kuongoza kikosi hicho kushinda mechi tatu mfululizo za ufunguzi wa msimu wa EPL.

Spurs wangalifunga mabao zaidi kupitia Steven Bergwijn, Eric Dier na Dele Alli ambao walishindwa kumzidi ujanja kipa Daniel Bachmann.

Spurs sasa wanajiandaa kuvaana na Crystal Palace, Chelsea na Arsenal katika msururu wa mechi tatu zijazo ligini. Kikosi hicho kilichoko chini ya ulinzi mkali wa Eric Dier na Davinson Sanchez bado hakijafungwa bao katika EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Everton kuachilia Moise Kean kurejea Juventus kujaza pengo...

MKU yapokezwa cheti maalum kwa kutambulika kama kituo rasmi...