Michezo

Tottenham wamsajili fowadi Vinicius kutoka Benfica kwa mkopo

October 2nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamejinasia huduma za fowadi Carlos Vinicius, 25, kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Benfica ya Ligi Kuu ya Ureno.

Kocha Jose Mourinho amekuwa akitafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kushirikiana vilivyo na nahodha Harry Kane kwenye safu ya mbele ya Tottenham ambao pia wanajivunia maarifa ya Son Heung-Min na sajili mpta Gareth Bale aliyetokea Real Madrid kwa mkopo.

Vinicius ambaye ni raia wa Brazil, aliwafungia Benfica jumla ya mabao 24 katika kampeni za Ligi Kuu ya Ureno muhula uliopita wa 2019-20.

Ingawa fowadi huyo wa zamani wa Napoli ya Italia ana kifungu kitakachomweka mnunuzi wake katika ulazima wa kuvunja benki ili kumsajili, Mourinho ana matumaini kwamba Tottenham watajitwalia kabisa huduma za Vinicius mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Itawajuzu Tottenham kuweka mezani kima cha Sh5.7 bilioni ili kurasimisha uhamisho wa Vinicius hadi kambini mwao kwa mkataba wa kudumu mwishoni mwa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO