Tottenham wapepeta Southampton 4-1 katika EPL

Tottenham wapepeta Southampton 4-1 katika EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Antonio Conte ametaka mashabiki kutarajia makuu zaidi kutoka kwa Tottenham Hotspur muhula huu baada ya kikosi chake hicho kukomoa Southampton 4-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Spurs walijinyanyua upesi baada ya Southampton kuwekwa kifua mbele na James Ward-Prowse. Kikosi hicho kinachopigiwa upatu wa kutamba msimu huu, kilipata mabao kupitia Ryan Sessegnon, Eric Dier, Dejan Kulusevski na Mohammed Salisu aliyejifunga.

“Japo tulizoa alama tatu muhimu, kubwa zaidi ni jinsi tulivyoshinda. Tulicheza kwa kujituma na kujiamini mno. Tulitamalaki mchezo kuanzia mwanzo na tukalemea washindani wetu katika kila idara,” akatanguliza Conte.

“Sioni chochote kitakachotunyima taji la EPL na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula huu iwapo tutaendelea kucheza namna tulivyofanya dhidi ya Southampton,” akaongeza mkufunzi huyo wa zamani wa Chelsea, Juventus na Inter Milan.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Spurs kuanza kampeni za EPL kwa ushindi mnono mbele ya mashabiki wao wa nyumbani tangu Disemba 2019 walipotandika Burnley 5-0.

Kwa mujibu wa Conte, ushindi dhidi ya Southampton ni onyo kali kwa wapinzani wao wakuu katika EPL na UEFA kwa kuwa masogora wake wana kiu ya “kuwapa mashabiki ‘kitu’ cha kufuatilia zaidi msimu huu.”

“Tumejishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho na tuna kila sababu ya kuwa mwiba kwa wapinzani na kushinda mechi nyingi iwezekanavyo katika mapambano ya muhula huu,” akasisitiza Conte.

Ilivyo, idadi kubwa ya wachezaji ambao Spurs wamesajili muhula huu inadhihirisha kiu ya Conte kuanza kunyanyulia waajiri wake mataji ya haiba chini ya kipindi kifupi iwezekanavyo.

Kufikia sasa, Spurs wamesajili wanasoka sita wakiemo Fraser Forster, Yves Bissouma, Djed Spence, Clement Lenglet, Ivan Perisic na Richarlison Andrade aliyetia saini kandarasi ya miaka mitano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Raha ikizidi sana si raha tena!

Mistari ya mwisho

T L