Na MASHIRIKA
TOTTENHAM Hotspur wamemsajili fowadi mzoefu Arnaut Danjuma kutoka Villarreal kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu wa 2022-23.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 anakuwa mchezaji wa kwanza kuingia katika sajili rasmi ya Spurs mwezi huu wa Januari 2023. Alikuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kuyoyomea kambini mwa Everton kabla ya Spurs kuanza kumvizia.
Danjuma aliwahi kuchezea Bournemouth kati ya 2019 na 2021 na akapachika wavuni mabao 17 kutokana na mechi 52 kabla ya kuyoyomea Uhispania kunogesha kipute cha La Liga.
Ingawa anajivunia kufungia Uholanzi mabao mawili kutokana na mechi sita, hakujumuishwa katika kikosi kilichotegemewa na timu hiyo ya taifa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.
Danjuma alitegemewa sana na Villarreal hadi nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021-22 na akafungia waajiri wake mabao 16 katika mashindano yote.
Kusajiliwa kwake kunaimarisha zaidi safu ya mbele ya Spurs ambayo tayari inajivunia maarifa ya wavamizi mahiri Harry Kane, Son Heung-min, Dejan Kulusevski, Richarlison Andrade na Lucas Moura.
Kufikia sasa, Spurs ya kocha Antonio Conte inashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 36, tatu pekee nyuma ya Manchester United na Newcastle United.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO