Michezo

Tottenham yabadua Chelsea nje ya Carabao Cup

October 1st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Mason Mount alipoteza penalti muhimu ambayo iliwawezesha Tottnham Hotspur kuwabandua Chelsea kwenye Carabao Cup mnamo Septemba 29, 2020.

Mshindi wa mechi hiyo iliyosakatiwa uwanjani Tottenham Hotspur Stadium aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote mbili kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1 mwishoni mwa dakika 90.

Jumla ya penalti tisa zilipigwa katika mechi hiyo kabla ya Mount aliyekuwa akichanja mkwaju wa 10 kugonga mhimili wa goli na mpira huo Kwenda nje.

Chelsea walitawala kipindi cha kwanza cha mchezo huo na wakafungiwa bao na sajili mpya Timo Werner kunako dakika ya 19. Goli hilo lilikuwa la kwanza kwa Werner aliyebanduka kambini mwa RB Leipzig ya Ujerumani mwishoni mwa msimu jana na kutua ugani Stamford Bridge.

Tottenham walirejelea kipindi cha pili kwa matao ya juu huku sajili mpya Sergio Reguilon alimfanyisha kipa mpya wa Chelsea, Edouard Mendy kazi ya ziada.

Presha ya Tottenham langoni pa Chelsea ilizalisha matunda dakika saba kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Ushirikiano mkubwa kati ya Reguilon na nahodha Harry Kane ulichangia bao la Tottenham waliosawazishiwa na Erik Lamela.

Kabla ya mechi hiyo, kocha Jose Mourinho wa Tottenham alikuwa amefichua kwamba Carabao Cup si shindano watakalolichukulia kwa uzingativu mkuu msimu huu hasa ikizingatiwa ugumu wa ratiba yao.

Ratiba ngumu ya Tottenham itawashuhudia wakisakata jumla ya mechi nne zijazo chini ya kipindi cha siku nane.

Baada ya kula sare ya 1-1 dhidi ya Newcastle United mnamo Septemba 27 kisha kuvaana na Chelsea mnamo Septemba 29, Tottenham kwa sasa wamepangiwa kuchuana na Maccabi Haifa katika Europa League mnamo Oktoba 1 kisha kuchuana na Manchester United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 4, 2020.

Mourinho ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Man-United, alipokezwa mikoba ya Tottenham mnamo Novemba 2019 baada ya kutimuliwa kwa Mauricio Pochettino ambaye ni raia wa Argentina.

Eric Dier, Lamela, Pierre-Emile Hojbjerg, Lucas Moura Kane walifunga penalti zao kwa upande wa Tottenham na kufuzu kwa robo-fainali za Carabao Cup zitakazoakatwa mnamo Disemba 2020.

Msimu wa kwanza wa Lampard kambini mwa Chelsea ulikuwa wa kuridhisha sana kiasi kwamba aliongoza kikosi hicho kutinga nafasi ya nne jedwalini licha ya kujivunia huduma za chipukizi pekee.

Aidha, walitinga fainali ya Kombe la FA ambapo walizidiwa maarifa na Arsenal kwa ushindi wa 2-1 uwanjani Wembley, Uingereza.

Hata hivyo, Chelsea wameanza kampeni za msimu huu vibaya licha ya kusajili wanasoka wa haiba kubwa kwa zaidi ya Sh35 bilioni.

Mbali na Werner aliyefungia Leipzig jumla ya mabao 34 msimu jana, Chelsea wamesajili pia beki Ben Chilwell, kipa Mendy, kiungo Kai Harvertz, fowadi Hakim Ziyech, beki Xavier Mbuyamba, kiungo Malang Sarr na beki Thiago Silva.

Baada ya kuwapiga Brighton 3-1 katika mechi ya kwanza ya msimu, Chelsea hawakusajili ushindi katika mechi mbili zilizofuata ligini. Walipigwa 2-0 na Liverpool uwanjani Stamford Bridge kisha kutoka nyuma kwa mabao 3-0 na kuwalazimishia limbukeni West Brom sare ya 3-3 mnamo Septemba 26, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO