NA MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
ALIYEKUWA ajenti wa Yaya Toure, Dimitri Seluk amekanusha madai kwamba alipokea malipo kisiri kutoka kwa klabu ya Manchester City inayokabiliwa na mshtaka ya udanganyifu kwa sasa.
Seluk alikuwa ajenti wa raia huyo wa Côte d’Ivoire aliyesaidia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Premia (EPL) kutwaa mataji kadhaa alipokuwa Etihad kati ya 2010 hadi 2018.
Toure aliisaidia Manchester City kushinda ubingwa wa EPL mara tatu, Kombe la FA mara moja na League Cup mara mbili.
Seluk ambaye kwa sasa hana uhusiano wowote na Toure ambaye ndiye kocha wa timu ya vijana ya Tottenham Spurs aliulizwa na waandishi wa michezo iwapo aliwahi kupokea malipo kutoka kwa Manchester City kwa njia ya siri alipokuwa ajenti wa nyota huyo mstaafu.
“Nafahamu vyema Yaya alilipa ushuru, na kufanya kila kitu kwa uwazi. Niko tayari kujitetea mbele ya tume iliyoundwa iwapo nitahitajika na nitasema ninayosema hapa sasa.”
Manchester City imewekewa mashtaka 100 ya udanganyifu ambayo huenda yakachangia klabu hiyo kupigwa marufuku kutoka ligi kuu ya EPL.
Mashtaka hayo yanahusiana na ukiukaji wa kanuni kwa misimu 14 ambapo uchunguzi umeonyesha jinsi klabu hiyo ilivyoficha rekodi za malipo ya wachezaji na makocha, pamoja na stakabadhi za matumizi ya kifedha kwa ujumla.
Lakini taarifa rasmi ya klabu hiyo imekanusha madai hayo, huku ikisisitiza kwamba ina ushahidi wa kutosha kujitetea.
Mabingwa hao watetezi wa EPL wanadaiwa kuvunja kanuni hizo kati ya 2009 na 2018 na wameshtakiwa pia kwa kosa la kubana taarifa muhimu tangu uchunguzi huo uanzishwe 2018.
Udanganyifu mwingine ni pamoja na kukiuka sheria zinazohitaji maelezo kama ya ujira wa makocha wao kuanzia 2009-2010 hadi 2012-2013, timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Roberto Mancini.
Viongozi wa soka nchini Uingereza wamedai kwamba klabu hiyo pia ilivunja sheria zinazohusiana na kanuni za UEFA, ikiwemo matumizi ya fedha (Financial Fair Play (FFP) misimu ya 2013-2014 na misimu ya 2017-2018, mbali na kuficha faida ya uendelevu.
Subscribe our newsletter to stay updated