Habari Mseto

Tovuti ya IEBC yakwama watu wakiomba kazi

December 19th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

TOVUTI ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikwama Jumamosi huku Wakenya wakijaribu kuomba nafasi 400 zilizotangazwa jana, za maafisa wa kukagua sahihi za BBI.

IEBC ilitangaza mwendo wa saa nne asubuhi kwamba inahitaji makarani hao 400 na dakika tano baadaye, ilikuwa vigumu kuingia huko.

Na wakati huo huo watu walilalamika kwamba Sh93.7m zilizopewa IEBC na hazina kuu kufanikisha ukaguzi huo ni nyingi “ikitiliwa maanani madaktari wamegoma kwa kukosa vifaa muhimu vya kazi na huku serikali inatumia mamilioni ya pesa kukagua saini za mchakato wa BBI.”

Akitangaza nafasi hizo za kazi, mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati alisema watakaoajiriwa ni wale tu “kutoka kaunti ya Nairobi na viunga vyake.”

Bw Chebukati alisema watakaofaulu kupata ajira hiyo watakuwa wanapokea Sh1,200 kwa siku.

Bw Chebukati alisema watakaoajiriwa lazima wawe raia wa Kenya walio na ufahamu wa masuala ya kompyuta na uingizaji wa tarakimu kwenye mitambo hiyo.

“Zoezi hili la ukaguzi wa saini hizi litaendelezwa Nairobi na watakaowasilisha maombi ya kazi hii lazima wawe ni wakazi wa kaunti hii na viunga vyake,” alisema Bw Chebukati.

Wanaowasilisha maombi ya ajira hiyo watatakiwa wajiandae kufanya kazi kwa masaa mengi na wafanye mipango yao ya usafiri na malazi.

Bw Chebukati alisema watakaofaulu ni wale watakaotuma maombi katika tovuti ya IEBC na wale watakaowasilisha barua kwa afisi hiyo hawatazingatiwa.

“IEBC itawasiliana na watatakaoteuliwa kufanya zoezi hili,” alisema Bw Chebukati.

Mwenyekiti huyo alisema hazina kuu ya kitaifa imeipa tume hiyo Sh93,739,800 kugharimia zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya watakaoajiriwa.

Baada ya kupokea sahihi hizo 4.4 milioni kutoka kwa kamati simamizi ya BBI, tume hiyo inatakiwa kuzikagua zote ihakikishe hakuna ufisadi umeingizwa katika zoezi hilo.

“Kwa mujibu wa Kifungu nambari 257(4) cha Katiba IEBC inatakiwa kukagua saini hizo kabla ya hoja kuwasilishwa katika mabunge ya kaunti kujadili kuhusu kufanyiwa marekebisho kwa katiba,” akasema.

Bw Chebukati alipokea ripoti yenye sahihi hizo mnamo Desemba 11, 2020.

Katika taarifa aliyotuma mnamo Desemba 18 2020, Bw Chebukati alisema mchakato wa BBI utaingia awamu nyingine ya ukaguzi wa sahini hizo kabla ya mabunge ya kaunti kuanza mjadala huo wa urekebishaji katiba.

Akiwasilisha bajeti ya Sh241 milioni kwa hazina kuu ya kitaifa, Bw Chebukati alisema zoezi hilo la ukaguzi wa saini hizo itatekelezwa na makarani watakaokodishiwa malazi kwenye mahoteli kuwakinga na athari za kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

“Kwa kuzingatia masharti yaliyotangazwa na wizara ya afya kuhusu Covid-19 tume hii itawakodishia makarani watakaokagua sahini vyumba kwenye mahoteli wasiambukizwe viini hivi vya corona wakisafiri kila siku kutoka makwao,” alisema Bw Chebukati.

Kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Ijumaa aliikashifu IEBC kwa kuitisha kiasi kikubwa cha pesa kuendesha kura ya maamuzi kuhusu BBI.