Habari Mseto

Kitoweo cha trafiki chamwagwa baada ya vizuizi kuondolewa barabarani

July 10th, 2020 1 min read

Na WAANDISHI WETU

POLISI wengi wa trafiki sasa watapoteza mfereji wa sehemu kubwa ya mapato yao kufuatia agizo la wakuu wao kuondoa vizuizi barabarani.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Edward Mbugua, alisema maafisa wengi wa ngazi za juu wamekuwa wakikaidi agizo lililotolewa mwaka uliopita na Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai.

Bw Mutyambai alikuwa ameamuru polisi wakome kuweka vizuizi barabarani kiholela.

Wakati huo, wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma walikuwa wanalalamika kupoteza mamilioni ya pesa wakilazimishwa kutoa hongo katika vizuizi vingi barabarani.

Kwenye barua iliyotumwa kwa wakuu wa vituo vya polisi, Bw Mbugua alisema polisi huwa wanafaa kupiga doria wala si kukaa barabarani.

Alieleza kuwa, maafisa wa trafiki wa ngazi za chini hutumiwa kukusanya hongo ambazo hugawana baadaye.

“Lengo lao kuweka vizuizi barabarani si siri. Huwa wanataka kujihusisha na ufisadi kwa manufaa ya makamanda na yao kibinafsi,” akasema.

Barabara ambazo huwa na idadi kubwa ya vizuizi vya polisi bila sababu ni barabara kuu za Nairobi-Mombasa, Nairobi-Nakuru na zile zinazoelekea maeneo ya magharibi mwa Kenya.

Kando na hayo, kuna vizuizi vingi ambavyo huwekwa pia katika barabara za mashinani kwa lengo hilo la kupokea hongo.

Shughuli hizi haramu huendelezwa peupe, na hata ufichuzi unapofanywa na wanahabari au mashirika ya kupambana na ufisadi, polisi husika huwa hawajali.

Hii ni mojawapo ya sababu ambazo hufanya idara hiyo kushikilia nafasi ya juu kwenye orodha za idara zinazokumbwa na ufisadi zaidi nchini.

Katika siku za hivi majuzi, idara ya polisi imekuwa ikimulikwa kutokana na jinsi Wakenya walifanikiwa kusafiri kutoka sehemu za miji na mitaa ambayo ilifungwa ikiwa na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Ilibainika maafisa ambao walipewa jukumu la kuzuia watu kuondoka katika maeneo hayo walikuwa wakipokea hongo kutoka kwa wananchi kisha kuwaruhusu kuendelea na safari zao.