Michezo

Trans Nzoia Falcons wasaka vipaji kuibuka kidedea

December 24th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA ni miaka mitatu tangu Trans Nzoia Falcons izaliwe imeibuka kati ya vikosi vilivyotifua vumbi la kibabe katika Soka la Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) ndani ya misimu miwili sasa.

Licha ya kupambana mwanzo mwisho vipusa hao waliokuwa wakitiwa makali na kocha, Evans Ingosi waliteleza na kushindwa kutimiza azimio la kumaliza kati ya tatu bora msimu wa 2018/2019.

NAFASI YA NNE

Wachana nyavu hao walijituma kisabuni na kuibuka nne bora katika jedwali la kipute hicho kwa kukusanya alama 64, nane mbele ya Kisumu All Starlets.

Trans Nzoia ilianza kampeni za kipute hicho kwa kishindo iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2018 ilikofanikiwa kumaliza tatu bora.

Vihiga Queens ambayo hunolewa na kocha, Alex Alumira alihifadhi taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo kwa kufikisha alama 79 baada ya kushuka dimbani mara 28. Gaspo Women ilimaliza ya pili kwa alama 70, mbili mbele ya Thika Queens.

Kati ya wachezaji wa Spedag FC. Picha/ John Kimwere

Nayo Kisumu All Starlets ilimaliza tano bora, Wadadia LG iliibuka ya nane huku Spedag ikimaliza ya mwisho nafasi ya 16 na kushushwa ngazi.

”Ninaamini kampeni za michezo ya muhula ujao itakuwa ya kukata mawimbi kiaina,” alisema kocha huyo na kuongeza kuwa timu zote zinajipanga kutifua vumbi la kufa mtu kwenye migarazano ya msimu ujao.

Aidha alisema kwa upande wao wanapania kusaka huduma za wanasoka wapya ili kujiweka vizuri kukabili wapinzani wao.

Kocha huyo anasema Kaunti ya Trans-Nzoia na Pokot zimefurika wachezaji wengi tu wanaotafuta timu za kuchezea ambapo swala la kusajili wachezaji wapya kamwe sio tatizo.

Baadhi ya wachezaji wa Wadadia FC. Picha/ John Kimwere

TUMAINI WALIAULA NA MARTHA AMUNYOLETE

Ndani ya misimu miwili kikosi hicho kimeonyesha soka la kutesa na kuvitia hofu timu zinazojivunia kushiriki kampeni hizo kwa muda.

Kando na vikosi vilivyoshusha upinzani mkali kwenye mechi hizo msimu ujao kipute hicho pia kitajumuisha wakali wa Kahawa Queens. Mchezaji wa Trans Nzoia Falcons, Tumaini Waliaula aliibuka miongoni mwa orodha ya wafungaji bora watano.

Msichana huyo aliye fundi wa mabao alifanikiwa kutupia kambani jumla ya mabao 30. Tereza Engesha aliibuka kileleni baada ya kuitingia Vihiga Queens jumla ya magoli 36.

Kati ya wachezaji wa Kisumu All Starlets. Picha/ John Kimwere

Kando na Tumaini Waliaula, inajivunia huduma za wachana nyavu matata kama Martha Amunyolete na Susan Muhonja kati ya wengine bila kuweka katika kaburi la sahau Valentine Cherop beki wa kuotea mbali.

Trans Nzoia inajumuisha wachezaji kama: Phylis Chemutai (kipa), Valentine Cherop, Naomi Wanjala, Monica Paul, Irene Khasanti, Cynthia Livondo, Joan Naliaka, Millicent Ayuma, Martha Amunyolete, Susan Muhonja na Lavender Jeddy.

Wengine wakiwa Mercy Fabbian, Caren Nangila, Lydia Chebet, Sharon Mukhwana, Linda Nasimiyu, Maureen Khakasa, Hellen Mulubi na Sofia Adhiambo.